MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imeahirisha kutoa hukumu ya shauri dogo lililofunguliwa na Wakili Tundu Lissu kupinga kesi namba 19525 mwaka 2024 inayomhusu Askofu Machumu Kadutu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam kwa kuwa hukumu haijakamilika.
Askofu huyo anashtakiwa kwa tuhuma za kutamka maneno ya uchochezi akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa siasa uliofanyika kata ya Ibaga, wilaya ya Mkalama, mkoani Singida.
Katika shauri hilo dogo, Lissu anaomba mahakama hiyo itupilie mbali shauri dhidi ya mteja wake kwa madai kuwa kesi hiyo haina mashiko.
Akiahirisha kesi hiyo jana hadi Desemba 16 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Allu Nzowa, alisema hukumu haijakamilika, hivyo mahakama inaendelea kuandaa.
Katika shauri hilo la jinai namba 19525 la mwaka 2024, Askofu Kadutu, kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka, anadaiwa kutamka maneno hayo ya uchochezi alipokuwa anahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 3, mwaka huu katika kijiji cha Ibaga, wilayani Mkalama.
Ilidaiwa mahakamani huko na Wakili wa Serikali Almachius Bagenda kuwa maneno aliyoyatoa mshtakiwa ni kosa kisheria na yanaweza kujenga chuki ya wananchi dhidi ya askari na serikali yao.
Wakili Bagenda alidai kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alitamka maneno: "...naweza kukosea njia wakati wa kwenda lakini huwezi kukosea njia wakati wa kurudi, mmeshaifahamu njia, walichofanya 2019 hakitajirudia... wangapi nyumbani mna majembe, wangapi mna visu nyumbani?
"Wangapi nyumbani mna panga...? Sasa mimi ninawaambia hivi; kama kupitia polisi... kama wamerudia tena katika uchaguzi ili wapitishe wanavyotaka wao, haki ya Mungu safari hii haya majembe yatakuwa na matumizi mengine... wakiwananii na nyie mnafanyaje? Mnawananiii..."
Alidai maneno hayo yaliyotamkwa katika soko la zamani, eneo la Madukani, kijiji cha Ibaga, ni kinyume cha sheria za nchi.
Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo, Wakili Hemedi Kulungu, anayemtetea mshtakiwa, alisema Lissu hakuwa mahakamani jana kutokana na kuwa kikazi nje ya mkoa wa Singida, anakoshiriki kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jijini Dar es Salaam.
Jopo la Mawakili wa Serikali linaongozwa na Almachius Bagenda, akisaidiana na Nehemia Kilimhana na Michael Martin wakati Lissu anasaidiwa na Hemedi Kulungu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED