JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, limewatembelea wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, na kuwapatia msaada.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mkuu wa Polisi Jamii mkoa huo, ACP Ally Wendo, amesema jeshi hilo limeona litoe msaada kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, likitambua uwapo wa wagonjwa ambao hawana uwezo kabisa.
“Zawadi hizi zimetoka kwa Polisi Mkoa wa Kinondoni, tumeona tutoe kile kidogo tulichonacho kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu wanaopata matibabu hapa, nimeambatana na OCD Kimara pamoja na OCS Kimara (Gogoni), tunaamini zawadi hizi zitaongeza matumaini kwao,” amesema ACP Wendo
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni (OCD) SSP Deogratias Massawe, amesema pamoja na kukabidhi msaada huo wamepata fursa ya elimu namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii hospitalini hapo, Emmanuel Mwasota, amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa msaada huo na kuongeza kuwa hospitali hiyo inapokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, huku wengine ni wanaopata ajali barabarani ambao wengi wao ndugu zao hawajulikani na hufikishwa hospitalini wakiwa hawana kumbukumbu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED