Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetaka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kutumia njia mbadala ya uchenjuaji na kuacha matumizi hatarishi ya kemikali ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu na Mazingira.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dk. Menan Jangu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na athari za matumizi ya zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira katika mkutano uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Baraza jijini Dar es Salaam.
Dk.Menan amesema takribani zaidi ya watu milioni 1.5 nchini wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ambao wengi wao wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni rahisi na bei nafuu katika shughuli za uchenjuaji madini lakini ina madhara makubwa kwa kusababisha magonjwa kama kansa, utindio wa ubongo na matatizo katika mfumo wa uzazi wa binadamu.
Amesema Baraza kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Mfuko wa GF wanaendelea kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya zebaki na linasisitiza shughuli zote za madini zifanyike katika utaratibu ambao hautakuwa hatarishi kwa jamii na mazingira.
Naye, Mratibu Mkuu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya zebaki (EHPMP) Mhandisi Dk. Befrina Igulu ameitaka jamii ichukue tahadhari ya matumizi ya zebaki ambayo ni hatari na endapo itatumiwa itumike kwa utaratibu maalumu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED