‘Makundi maalum changamkieni zabuni serikalini’

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:44 AM Jul 01 2024
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa.
Picha: Mpigapicha Wetu
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa.

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, amewataka wanawake, vijana na wenye ulemavu, kuchangamkia zabuni za serikali kwa kuwa asilimia 30 ya bajeti yote ya ununuzi wa umma, imetengwa kwa ajili ya makundi hayo.

Beng’i aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizindua Programu ya BID for success (B4S), inayoratibiwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), kwa lengo la kuwajengea wanawake na vijana uwezo wa kushiriki zabuni za serikali, kwenye sekta mbalimbali.

Alisema ununuzi wa umma unatumia asilimia 80 ya bajeti ya matumizi ya serikali, akieleza kuwa asilimia 30 inayotajwa kwenye kanuni za Sheria ya ununuzi ya umma inafikia Shilingi trilioni mbili kwa mwaka.

“Kama tutazipata zikaingia kwenye biashara zetu zitachochea sana ukuaji wa uchumi wenye matokeo makubwa. Nataka niwape hiyo changamato wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na wazee kwamba turasimishe biashara zetu ili tuweze kuteka hizi fursa,” alisema.

Alisema makundi hayo yanapaswa kuzingatia utunzaji wa kumbukumbu za biashara, ubora, kuwa na uwezo wa kutoa huduma baada ya makubaliano na kutumia teknolojia kuingia kwenye mifumo ya kuomba zabuni.

“Mnaweza kujiunga kwenye umoja kwa muda fulani ili kuomba zabuni, hii itawasaidia kumudu zabuni kubwa. Zabuni inaweza kukuambia upeleke kiasi fulani kila wiki au mwezi na usiishiwe, umoja utatusaidia kuzalisha kwa wingi na kwa ubora ule ule. Tukiweza kufanikiwa kwenye ubora na uwezo wa kulishika soko, tutaweza kuingia kwenye masoko ya ndani na ya nje,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, alisema utafiti wa chemba hiyo wa mwaka 2021, ulibaini kwamba wanawake, vijana na makundi maalumu yanayoshinda zabuni za serikali ni chini ya asilimia mbili.

“Kwenye mpango wa B4S tunalenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana ili wakashindane kwenye zabuni na kuonyesha matokeo. Tunataka kuona ongezeko la wanawake kutumia hii fursa. Kwa mfano, wakati fulani, Wizara ya Ujenzi ilitangaza zabuni ambayo ilitenga Sh. bilioni 80 kwa ajili ya kampuni za wanawake, ni wanawake sita tu ndio waliomba…hii inatupa picha kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya,” alifafanua. 

Mkurugenzi Mkuu wa Trade Mark Afrika, Elibariki Shammy, alisema ili kusaidia vijana na wanawake, serikali inapaswa kulipa wazabuni kwa wakati.

“Serikali isipowalipa kwa wakati, kampuni hizi zitakufa mapema na lengo la kuwainua halitafikiwa,” alisema.

Alisema serikali inapaswa kuwa na sera madhubuti ya kukuza viwanda vya ndani, ili wazawa wanaposhinda zabuni, mzunguko wa fedha ubakie kwenye uchumi nchini.

Kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi ya Umma (PPRA), sura na 410 ya mwaka 2023 kifungu cha 64, halmashauri na ofisi zote za serikali zinapaswa kutenga bajeti yake ya ununuzi kila mwaka kwa ajili ya wazabuni wanawake, vijana na makundi maalumu.

Kanuni za sheria hiyo (PPR), ambazo zitaanza kutumia mwaka huu wa fedha 2024/2025, zinazitaka ofisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.