KAMATI ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imetembelea Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na baadhi ya viwanda vinavyosimamiwa na OSHA lengo likiwa ni kujifunza mfumo wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya kwa upande wa Tanzania Bara ili kushauri maboresho stahiki kwa upande wa Zanzibar.
Ziara hiyo imejumuisha wajumbe wa Kamati tajwa pamoja na watumishi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini iliyopo ndani ya Ofisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji-Zanzibar.
Ujumbe huo ulifika Ofisi za OSHA Dar es Salaam na kupata wasilisho kuhusu utendaji wa taasisi toka kwa Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda, ikiwemo hatua ambazo taasisi hiyo imepitia kutoka kuwa Idara ya Ukaguzi wa Viwanda katika Wizara yenye dhamana ya Masuala ya Kazi hadi kuwa taasisi inayojitegemea.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mtumwa Peya Yusuph, alisema wanatambua kwamba OSHA Tanzania Bara ipo mbali katika usimamizi wa masuala husika jambo ambalo limewasukuma kuja kujifunza ili kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuboresha mfumo wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya kwa upande wa Zanzibar.
“Tunatambua kwamba wenzetu huku bara mnafanya vizuri sana katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi hivyo tumeona ni busara kuja kujifunza ili tuweze kuchukua mazuri yaliyopo na tuishauri Serikali yetu kuyafanyia kazi,” alieleza Mwenyekiti huyo wa Kamati na kuongeza:
“Tunawapongeza sana OSHA kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuboresha usalama na afya kwenye maeneo ya kazi nchini kama tulivyoona katika wasilisho la Mtendaji Mkuu pamoja na hali halisi ya utekelezaji wa miongozo ya OSHA kwenye viwanda tulivyotembelea ambapo tumeona wahusika wamejitahidi kuzingatia taratibu muhimu za usalama na afya kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi.”
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA,Khadija Mwenda, alisema ziara hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya biashara na uwekezaji kote Tanzania Bara na Zanzibar kutokana na uhalisia kwamba wawekezaji wengi wamewekeza bara na visiwani na hivyo ni muhimu kuwa na mifumo na sheria zinazoendana.
“Tumeshasaini hati ya mashirikiano na wenzetu wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar hivyo tupo tayari kushirikiana nao katika kufanya maboresho wanayokusudia ili kama nchi tuwe na mifumo na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa,” alieleza Mwenda.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar,Ame Faki Saleh, alisema wanayo matumaini kuwa kupitia mashirikiano na OSHA Bara ambayo imeshapiga hatua kubwa katika usimamizi wa usalama na afya watajifunza mambo mengi yatakayosaidia kufanikisha safari ya mabadiliko ya Idara yao kuwa Taasisi inayojitegemea kwa upande wa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni za Bakhresa, ambako ni miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na Kamati,Hussein Sufiani alitoa ushuhuda kwamba kampuni za Bakhresa zimepata mafanikio makubwa katika biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na kutekeleza ipasavyo sheria za nchi ikiwemo miongozo ya OSHA kuhusu usalama na afya kazini.
Ziara hiyo ya Kamati inafanyika kwa siku mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ambapo maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Kiwanda cha Berger Paints International Ltd na Kiwanda cha Unga cha Bakhresa (Dar es Salaam) pamoja na Kiwanda cha Mbolea cha Intracom na Mji wa Serikali Mtumba (Dodoma).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED