Biteko ataka mkakati kuinua makandarasi

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:37 AM Jul 01 2024
NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, ameielekeza Wizara ya Ujenzi kuweka mkakati wa kuwainua makandarasi nchini, pamoja na mpango mzuri wa taasisi za fedha kuwakopesha ili wakuze mitaji yao.

Aidha, amesema makandarasi hao wakikuza mitaji yao watajenga miradi mikubwa kama wenzao wa nje.

Aliiagiza wizara hiyo kutekeleza mkakati huo ipasavyo kuanzia ngazi ya Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Fedha.

Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga kongamano la makandarasi na watoa huduma, lililoandaliwa na Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA). 

Alisema katika mpango mkakati wa kukuza makandarasi wa ndani kuwekwe kipengele cha kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za mikopo kutoka kwa wadau wa maendeleo kunatengwa asilimia isiyopungua 20 kwa ajili ya makandarasi wa ndani.

Aidha, alisema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na alitoa maelekezo kwa viongozi wote wa serikali pamoja na watumishi wa ngazi zote kuhahakikisha wanatekeleza agizo hilo.

Kadhalika, Dk. Biteko aliwataka makandarasi nchini kutekeleza miradi ya ujenzi kwa ubora na uzalendo mkubwa, ili wainue uchumi wa nchi na kuhakikisha wanatekeleza miradi mikubwa.

Pia, aliwataka waheshimu matumizi ya fedha za miradi, kwa kufanyia shughuli za ujenzi na faida watakayoipata waiwekeze kama mkakati wa kukuza mitaji ya kampuni zao.

Alisema ofisi ya waziri mkuu itaelekeza sekta zingine zikiwemo za nishati, maji na uchukuzi, kuhakikisha zina wapa upendeleo makandarasi wazawa pamoja na kuwawekea malengo.

Alisema kwenye mikutano yao ya kila mwaka wapime utekelezaji wa malengo hayo na kama kuna changamoto basi waweke mikakati ya kuzitatua ili waweze kukua kwa haraka.

Aidha, aliitaka wizara ya ujenzi kuiga mfano wa kuwaendeleza vijana wa wizara ya kilimo uitwao ‘Build Better Tomorrow’ (BBT), kwa kuwasaidia vijana kuanzisha kampuni na kuwapatia kazi ndogo ndogo ili kuwajengea uzoefu.

Dk. Biteko pia alisisitiza kuwa serikali imeendelea kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

"Napenda niwahakikishie kuwa serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watumishi wanaojihusisha na rushwa. Ombi langu kwenu mnapokutana na tatizo la rushwa msisite kutoa taarifa TAKUKURU," alisema Dk. Biteko.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alisema Rais Samia anatambua mchango wa makandarasi wazawa nchini na anataka kuona wanakuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.

Mwenyekiti wa TUCASA, Samwel Marwa, aliiomba serikali iwe mlezi kwa TUCASA, ili kuwajengea uwezo wa kufanya miradi mikubwa ya ujenzi kwa kuisimamia wenyewe.

Pia aliiomba serikali kuendelea kupambana na rushwa ili makandarasi wazawa wapate zabuni kubwa za ujenzi na hatimaye kukuza kampuni zao.