RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilipata wabunge 115 na madiwani wengi kwa sababu ya umaarufu na kukubalika kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.
Lowassa alikuwa kiongozi mlezi ambaye aliwalea vijana wengi kwenye siasa ambao kwa sasa wanaendelea kulitumikia taifa na sifa hii ya ulezi kwa vijana ilimjengea umaarufu na mapenzi makubwa kwa wananchi Ndiyo maana alichosema hata mdogo wangu Freeman Mbowe yale matokeo ya zile kura ni kwa sababu ya Lowassa ambaye alijenga umaarufu mkubwa sana yeye mwenyewe binafsi na siyo chama chao, ndiyo sababu umekuja na kupata kitu cha kusema”. amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Lowassa aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam, alizikwa jana nyumbani kwao, Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza katika maziko ya kiongozi huyo, Rais Samia amesema idadi hiyo ilichangiwa na mambo mengi na mzuri aliyofanya (Lowassa) kwenye jamii na kwa taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo baada kuibuliwa hoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, kwamba haiwezekani kuitenga, kuandika au kurekodi mazuri aliyoyafanya Hayati Lowassa pasipo kukitaja chama hicho cha upinzani.
Mbowe amesema taifa limepoteza mmoja wa viongozi mahiri, mpenda maendeleo, mwana mageuzi na kipenzi cha watu wengi na alitoa pole kwa familia na wananchi na Watanzania kwa msiba huo.
Samia amesema: “Wasifu wa Lowassa alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na serikalini hadi kufikia nafasi ya Waziri Mkuu na nusu ya maisha yake ametumia katika utumishi na uongozi wa umma. Alijitolea muda wa maisha yake kwa ajili ya nchi yake kwa kubeba dhamana kwa kila sehemu alipokabidhiwa.
Amesema Lowassa alipokuwa mgombea wa urais mwaka 2015 aliweka wazi kwamba kipaumbele chake cha kwanza kilikuwa elimu, pili elimu na cha tatu elimu kwa sababu alipenda vijana wapate elimu, maarifa na ujuzi kwa ajili ya ustawi wa familia zao na jamii kwa ujumla.
“Lowassa alikuwa muumini wa elimu kama nyenzo ya kujikomboa na umasikini na mara zote alisisitiza kuwa haupendi umasikini, nakumbuka aliwahi kusema nimekuwa na nitaendelea kupambana na kusisitiza elimu bora ambayo inawaandaa vijana kuingia kwenye soko la ajira,” amesema Samia.
Pia amesema imani na msimamo wa Lowassa vilisukuma na kusimamia kwa mafanikio mpango wa maendeleo wa elimu ya sekondari akiwa Waziri Mkuu.
Amesema mpango huo ulianza kuongeza wanafunzi wanaopata elimu ya sekondari kwa utaratibu sambamba na kusimamia ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata nchini, licha ya kuwapo kwa maoni kinzani kutoka kwa baadhi ya wadau wa elimu.
Vilevile amesema Lowassa alikuwa kiongozi jasiri, shupavu na mstahimilivu na mlezi kwa kila jambo alilokuwa akifanya wakati akiwa serikalini na kwenye CCM.
“Ndugu yetu Lowassa alikuwa kiongozi jasiri na shupavu na alionyesha ushupavu katika nyakati mbalimbali wakati wa uongozi wake kwa kuwa alisimamia mambo yaliyokubalika ndani ya serikali na yale aliyoagizwa na chama bila kutetereka. Mfano alipokuwa Waziri wa Maji na Uvuvi licha ya kuwapo kwa shinikizo la kutokutumia maji ya Ziwa Victoria kwa sababu za kihistoria kwa ujasiri na ushupavu aliishauri vema serikali,” amesema.
Sambamba na hayo, alisema pia amesema Hayati Lowassa atakumbukwa kwa usimamizi na ufuatiliaji wa mamlaka za maji za miji mikuu ya mikoa zilizoleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za maji safi na salama na uondoaji wa maji taka.
“Jambo la kujifunza ukipewa dhamana ya uongozi au kuaminiwa katika nafasi mbalimbali ni lazima tuwe na uthubutu na ubunifu pamoja na kusimamia na kutekeleza maelekezo ya serikali bila ya kukubali kuyumbishwa,” amesema.
ALICHOSEMA MBOWE
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amesema haiwezekani kukitenganisha chama hicho na historia ya Hayati Lowassa kwa kuwa akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA alikuwa karama ya kuunganisha watu hasa vijana na kuwalea.
Amesema Lowassa alikuwa mwana demokrasia na alichangia sehemu kubwa ya chama hicho kupata viti 115 vya ubunge na madiwani zaidi ya 2,000 wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015.
“Wakati akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA alikuwa ni mtu mnyenyekevu anayependa kusikiliza na kuonyesha njia, kadhalika alikuwa kiunganishi na kipenzi cha watu wengi kwa kuwa hakuwa mbaguzi,” amesema Mbowe.
Akizungumza kwa niaba ya familia, mtoto wa Hayati Lowassa, Fredrick Lowassa, amesema maisha ya baba yao yalikuwa tunu na nyota iliyong’aa ndani ya CCM na alipokuwa mtendaji na mtumishi serikalini.
“Itakuwa ni mtihani mkubwa kwa familia yetu kuvaa viatu vyake kutokana na hekima aliyokuwa nayo pamoja na uhodari wake. Ila tunashukuru Mungu kwa zawadi yake kipindi chote alichoumwa hadi mauti yalipomfika,” amesema Fredrick.
MAJALIWA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema baada ya msiba huo kutokea Rais Samia alitoa maelekezo ya kwa Kamati ya Maafa Kitaifa kuhakikisha kuwa wanafanya maandalizi vizuri ya msiba ili Hayati Lowassa azikwe kwa heshima.
“Naipongeza kamati kwa usimamizi wa kazi hii wamefanya kazi nzuri kwa kuwa shughuli imekwenda vizuri mpaka tulipotamatisha leo (jana), pia niwashukuru wananchi wote kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kwa kujitokeza kwa siku tano kwenye maombolezo ya kuaga mwili wa mpendwa wetu,” amesema .
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia hiyo kwa niaba ya wabunge, huku akisisitiza kuwa neno la wabunge linatoka kwenye biblia kitabu cha Wagalatia 6:7.
“Pamoja na biblia kutueleza kuwa siku zetu za kuishi hapa duniani ni chache na tukichanua tunakatwa kama maua basi tuna nafasi ya kuwa maua mazuri yanayochanua na kutoa harufu nzuri,” amesema Dk. Tulia na kuongeza:
“Kitabu cha Wagalatia 6.7 kinasema msidanganyike kwa kuwa Mungu adhihakiwi, hivyo usidanganyike kwa kuwa upandacho ndicho utakachovuna.”
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema Hayati Lowassa alikuwa sehemu ya mwana maendeleo kwa mkoa huo na jamii kwa ujumla, hivyo alisisitiza kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kwa familia hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED