Waziri Mkuu aipa kibarua TAKUKURU

By Mary Mosha , Nipashe Jumapili
Published at 08:41 AM Oct 27 2024

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa.
Picha:Mtandao
WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa, ametoa maagizo matatu kwa maofisa wapya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), akitaka wawe wakali katika mifumo ya ununuzi wa umma, utoaji wa ajira na ukusanyaji wa mapato.

Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, aliyasema hayo jana mjini hapa katika Shule ya Polisi wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa maofisa 436 wa TAKUKURU.

Alisema  katika maeneo hayo, bado kuna matatizo makubwa na kuwataka kutumia ujuzi walioupata pamoja na sheria, ili kutokomeza wala rushwa nchini.

“Ninyi si maofisa wa kukaa ofisini. Nendeni  kwa wananchi, waelimisheni kuhusu rushwa na madhara yake. Watumieni wanasiasa wakiwamo madiwani na wabunge katika  kuwapata wananchi. Tukatae rushwa.

“Wako watu wanaokosa huduma za afya, elimu  na maji, hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha rushwa inageuka historia hapa nchini," alisema.

 Majaliwa aliitaka Wizara ya Elimu, Sanyansi na Technologia kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuendelea kukamilisha mchakato wa usambazaji wa vitabu maalumu kwenye shule zote, ili somo la historia na maadili ya Mtanzania lianzie kufundishwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2025.

“Sera mpya inaeleza lengo la serikali ni kujenga uzalendo na maadili ya nchi ikiwa ni sehemu ya kuchukia rushwa,” alisema.

Majaliwa aliwataka kwenda kusimamia fedha zinazotolewa serikali katika miradi mbalimbali  na kuwaainisha wala rushwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene, aliwataka watumishi hao kufanya kazi itakayosaidia taifa.

“Mna bahati sana. Mliomba kazi, mmepata kazi. Kafanyeni  kazi eneo lolote mlilopangwa, kawajibikeni na mlete mabadiliko,” aliagiza.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema serikali imeendelea kuboresha vitendea kazi katika taasisi hiyo na kwa sasa watafanya kazi kwa weledi mkubwa na hawatakuwa na kisingizio chochote.

Chamamila alisema serikali imeshatoa Sh. bilioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa magari mapya 195 na hadi sasa yameshanunuliwa magari 88 yatakayosambazwa katika ofisi mbalimbali za TAKUKURU wilaya na mikoa nchini.