NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amezindua taarifa za utendaji katika sekta ndogo za umeme, gesi asilia na mafuta kwa mwaka 2022/ na kutoa maelekezo mahsusi kwa wizara na taasisi mbalimbali kufanyia kazi taarifa hizo zinazoonyesha mafanikio na changamoto katika sekta ya nishati.
Akizindua taarifa hizo juzi jijini Dodoma, Dk. Biteko aliziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, kusoma taarifa hizo na kuzichambua na changamoto zilizoainishwa zipatiwe majawabu ndani ya miezi mitatu.
Pia aliagiza kuwa kila aina ya fursa iliyoonekana kwenye taarifa hizo, ichukuliwe kwa uzito mkubwa na itambuliwe nani ana uwezo wa kuitumia fursa hiyo ndani ya serikali na taasisi binafsi.
“Vilevile nawaagiza EWURA (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) tathmini ya mwaka ujao ihusishe utendaji wa nishati safi ya kupikia ili kujipima kwa usahihi kuhusu utekelezaji wa ajenda hii inayopewa kipaumbele na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Aidha, Dk. Biteko aliagiza kuwa matishio yote ya sekta ya nishati yaliyoainishwa katika ripoti kati ya mwaka 2023 na 2025 yapatiwe suluhisho ili katika ripoti ijayo changamoto husika likiwemo suala la kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila mwaka lisiwapo.
Dk. Biteko pia aliitaka EWURA kupima uhusiano wa rasilimali zilizopo na mafanikio ya watu huku akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta lazima yaendane na mabadiliko ya maisha ya watu.
Kadhalika, alitaka mifumo ya uagizaji mafuta iendelee kuboreshwa baada ya kufanyika utafiti wa kina na kubainisha kwamba miundombinu ya mafuta bado inahitajika. Aliagiza kuachwa kwa urasimu katika sekta ya nishati.
Dk. Biteko aliipongeza EWURA kwa tathmini ambayo inaonyesha kuwa sekta ya nishati inaendelea kuimarika. Alitoa mfano wa kutolewa kwa leseni ya kuchimba gesi asilia katika kisima cha Ntorya mkoani Mtwara kitakachotoa futi za ujazo milioni 140 kwa siku na kwamba leseni ya mwisho ya kuchimba gesi ilitolewa mwaka 2006.
Kuhusu sekta ndogo ya umeme, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuiboresha ukiwamo mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao umeingiza mtambo wa pili katika gridi ya taifa kupitia mtambo namba nane, hivyo kufanya kiasi kilichoingia hadi sasa kuwa megawati 470.
“Sekta binafsi imetutoa kimasomaso. Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme. Wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa na kwa taasisi zilizo chini ya wizara, msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alimshukuru Rais Samia kwa kuiimarisha sekta ya nishati huku akisema Dodoma imeshuhudia matunda ya uimarishaji huo wa sekta kwani sasa umeme haukatiki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema tathimini iliyozinduliwa inaonyesha sekta imepiga hatua kwenye maeneo megi ikiwamo uhakika wa upatikanaji umeme pamoja na upatikanaji na usambazaji wa mafuta.
Alisema upatikanaji na uwekezaji wa gesi unaendelea kuimarika ikijumuisha usambazaji gesi kwenye maeneo mbalimbali kama magari, majumbani na viwandani.
Akitoa taarifa za utendaji katika sekta ya nishati, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, alisema sekta hiyo inaendelea kuimarika ikiwamo uwekezaji kwenye miundombinu ya mafuta na uwekezaji wa vituo vya mafuta na maghala. Alisema kwa sasa kuna ongezeko la uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) kwa asilimia 16 na ongezeko la uagizaji wa mafuta kwa asilimia nane.
Dk. Andulile alisema kwa upande wa umeme, uwekezaji umeongezeka katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji huku akibainisha kuwa upotevu wa umeme unazidi kupungua na wateja wameongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2021/22 hadi milioni 4.4 mwaka 2022/23.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED