RIPOTI MAALUM: Wahitimu la saba wanavyobeba jukumu la wazazi kusaka fedha

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:13 AM Oct 06 2024
news
PICHA: NEEMA EMMANUEL
Mhitimu wa darasa la saba, Melison Samwel akichota maji katika moja ya visima, wilayani Magu, mkoani Mwanza, kwa ajili ya kwenda kuyauza katika migahawa na makazi ya watu. Hununua madumu tisa kwa bei ya 300/- na kuyauza kwa 2,000/-.

NI hatua mojawapo ya safari ya maisha katika elimu. Safari hiyo ni kuhitimu elimu ya msingi na kuanza maandalizi ya kuanza elimu ya sekondari. Kufikia hatua hiyo ni mafanikio na furaha kwa mwanafunzi na wazazi.

Lakini kwa kufikia hatua hiyo na kusubiri ifikapo Januari, mwakani, kuanza elimu ya sekondari mtoto anafanya nini? Hilo ni fumbo kubwa na wajuao ni wale wanaomzunguka. 

Wakati hali ikiwa hivyo, siku kadhaa baada ya wanafunzi hao kumaliza mitihani yao, katika maeneo kadhaa ya Kanda ya Ziwa, wamerejea nyumbani na kuanza shughuli mbalimbali za kusaka fedha. Lengo ni kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya masomo ya sekondari.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya kukwamisha ndoto za watoto hao kutokana na kukosa muda wa kujiendeleza na masomo ya utangulizi ya kidato cha kwanza (pre form one) na kuishia mitaani wakiuza mboga, matunda na kufanya shughuli za kuuza dukani na ajira za muda.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya wahitimu wanaofanya biashara mbalimbali, wamesema badala ya kusoma masomo ya awali ya kujiandaa kwenda kidato cha kwanza inawalazimu kufanya biashara ili kupata fedha za maandalizi kwa ajili ya kidato cha kwanza.

Mhitimu katika Shule ya Msingi Nyihogo, Kahama mkoani Shinyanga, Salome Richard, anasema anaamini atafaulu mtihani wa kuhitimu darasa  la saba na kuendelea na masomo isipokuwa anasaidiana na wazazi wake kufanya biashara ndogo ndogo za kuuza mboga mitaani ili kupata fedha za kununua mahitaji ya shule atakayopangiwa. 

Anasema kuna wakati wanapata changamoto ya kuitwa ndani na wanaume kuuza mboga na kuanza kushawishiwa kwa kupewa fedha ambazo zinazidi thamani ya mzigo walio nao na wale wasiojisimamia wanakubali na kuingia kwenye ngono zembe. 

Naye Kevin Bundala, mhitimu wa darasa la saba Shule ya Msingi Nyashimbi wilayani Kahama, anasema ugumu wa maisha katika familia yao ndiyo sababu ya kushirikiana na wazazi kufanya biashara hizo. Anasema wakikaa nyumbani wanaweza kujiingiza kwenye vitendo viovu vikiwamo matumizi ya dawa za kulevya na ngono.  

Mhitimu mwingine kutoka Magu mkoani Mwanza, Melison Samwel, anasema  kwa sasa anajihusisha na uuzaji wa maji na kuwa ananunua toroli lenye madumu tisa kwa Sh.300 na kuuza mitaani kwa Sh.2,000, hivyo kujipatia faida ya Sh.1,700 kwa tripu moja. 

"Kwa siku nina uwezo wa kupata tripu zaidi ya tano. Wateja  wangu ni watu wa hotelini na kwenye nyumba za watu. Nilianza  tu nilipomaliza shule. Fedha  ninazopata natunza kwa ajili ya kuwasaidia wazazi kununua baadhi ya vifaa vya shule endapo nitachaguliwa,” anasema. 

Kuhusu masomo ya awali ya sekondari Samwel anasema bado hajaanza kwa kuwa ni lazima alipe fedha kabla ya kuanza na uwezo wa wazazi wake kifedha si mzuri. Anasema baada ya shughuli zake za kila siku, wakati mwingine anamtumia dada yake ambaye yuko kidato cha tatu kumweleza baadhi ya mambo yaliyoko sekondari. 

MZAZI AFUNGUKA 

Baadhi ya wazazi wenye watoto wanaojihusisha na shughuli za utafutaji wakisubiri kuanza kidato cha kwanza, akiwamo Suzana Albogasti, alisema ni wakati wa mtoto wake ambaye kwa sasa anauza dukani kumsaidia katika kutafuta fedha za kidato cha kwanza. Anasema hali hiyo itamsaidia kutokujiunga na makundi yasiyo salama kitabia. 

“Nashukuru amemaliza vyema hivyo siwezi kuruhusu aanze kuzurura ovyo. Dunia  ya sasa imeharibika ni bora anisaidie kutafuta hela. Nina  imani atafanya vizuri akianza masomo,” anasema.

 WADAU WANENA

Diwani wa Bukandwe, Magu mkoani Mwanza, Marco Minzi, anawashauri  wazazi na walezi wa wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi kutenga muda wa watoto wao kufanya shughuli za nyumbani na muda wa kujisomea kwa ajili ya maandalizi ya hatua nyingine ya elimu ya sekondari. 

Anasema wakati huu si sahihi kwa mtoto kupatiwa majukumu ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kulima, kufanya biashara na kuchunga mfugo hali inayomfanya mtoto kusahau wajibu ulioko mbele yake wa kuendelea na masomo ya sekondari. Anasema ni wajibu wa mazazi na mlezi kuhakikisha anatenga muda wa mtoto kufanya shughuli hizo na kupata muda wa kutosha wa kujisomea. 

Meneja wa Shule ya Rwepa’s iliyoko Mhungula Manispaa ya Kahama, Frank Samweli, alisema kipindi chote cha shule walikuwa wakiwafundisha watoto maadili mema ili watakapokuwa uraiani wasije kujiingiza kwenye vitendo viovu na sasa jukumu la malezi libaki kwa wazazi na walezi, hivyo wana wajibu wa kuwaandaa na masomo ya mbele na sio kuwatwisha majukumu. 

Mwanasheria na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (SHIHABI), Onesmo Daudi, anasema mzazi haruhusiwi kubebesha majukumu mtoto kwa mujibu wa sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na endapo atabainika atachukuliwa hatua za kisheria. 

“Mtoto anapotumikishwa pindi amalizapo darasa la saba au kidato cha nne, anajiona kama ndio mwisho wake wa elimu na matokeo kusahau ndoto zake za kielimu. Tuache  kubebesha majukumu watoto yanayopaswa kubebwa na watu wakubwa wasio wanafunzi,” anasema Daudi. 

Ofisa Elimu Sekondari Manispaa ya Shinyanga, Lucas Mzungu, anawaagiza maofisa elimu kata kuwasaka na kuwapeleka shuleni wanafunzi wote ambao wamehitimu elimu ya msingi ambao wamekuwa wakizurura mitaani, ili wasome masomo ya Kiingereza  kwa ajili ya kujiandaa na kidato cha kwanza mwakani.

Anasema hali ya watoto kuendelea kuranda mitaani na hata kuuza vyakula ni hatari kwa maandalizi ya kuingia kidato cha kwanza.

Anasema utaratibu wa serikali ambao ulianzishwa ni kwamba wanafunzi ambao wamehitimu elimu ya msingi, wanapaswa kuanza masomo ya Kiingereza katika shule ambazo ziko jirani badala ya kuzurura mitaani au kujishughulisha na biashara ndogo ndogo.

“Wakasome masomo hayo tena bure kwa shule ambazo wako jirani nazo. Hii itasaidia kumwandaa mtoto vizuri na maandalizi ya kidato cha kwanza,” alisema Mzungu.

 Imeandaliwa na Neema Emmanuel (MWANZA), Elizaberth Faustine (MWANZA), Vitus Audax (MWANZA), Marco Maduhu (SHINYANGA), Shaban Njia (KAHAMA)