Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amewataka vijana nchini badala ya kuuliza nini nchi iwafanyie, ni vema wajiulize wao wataifanyia nini nchi yao.
Nyalandu ameyasema hayo leo Jumapili, Oktoba 20, 2024 alipohutubia wakati wa ufunguzi wa Baraza la Vijana lililopewa jina la Samia Love jijini Mbeya.
Amesema Taifa la Tanzania litajengwa na Watanzania wenyewe, hivyo ni vema kwa vijana kwa pamoja wajiulize nini wataifanyia Tanzania.
Hata hivyo, amesema umuhimu wa swali hilo kwa vijana unatokana na ukweli kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuiweka nchi katika mwelekeo mzuri.
Nyalandu amesema kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameiletea heshima Tanzania ni wajibu wa vijana kuona nini watalifanyia Taifa.
Katika hotuba yake hiyo, ameeleza Rais Samia aliyoifanyia Tanzania, akiwakumbusha vijana nao kutekeleza jukumu la kuifanyia nchi yao mambo mbalimbali, badala ya kulalamika.
“Itakumbukwa Rais Samia aliyesimama katika nyakati mahsusi alizopewa na Mungu na aliwatazama Watanzania katika tofauti zao.
“Akaamua kusimama katikati ya wote na kuwa mpatanishi, huku akiendelea kuifungua nchi ndani na nje ya mipaka,” amesema.
Amesema Mkuu huyo wa nchi ameliletea taifa heshima katikati ya chuki ambazo tayari zilishaanza kuingia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED