WATOTO wa mamalishe wenye umri kuanzia miaka sifuri hadi saba, ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini katika mmomonyoko wa maadili. Hali wanazopitia katika biashara za mama zao wanaoshinda nao barabarani.
Mkoani Tabora, karibu kila migahawa mitano, minne kuna mtoto wa mamalishe. Huamshwa alfajiri kila siku na kwenda na mama zao katika shughuli hizo.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe Jumapili, umebaini kundi hilo limekuwa likilelewa na kupata makuzi katika mazingira hatarishi kwa ustawi wa afya, maadili na hujifunza lugha za matusi, udakozi na uzururaji.
Mohamed Nassoro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tabora, anakiri kushuhudia hali hiyo mara kadhaa.
Anasema licha ya kuwaweka katika hatari watoto hao, wateja pia wako hatarini kutokana na tabia za watoto hao kujisaidia ovyo. Nassoro anasema kuna haja ya serikali kulitazama tatizo hilo na kuona namna ya kukabiliana nalo, kwa ajili ya mustakabali wa maisha ya watoto hao.
“Hili ni tatizo kubwa na linatakiwa kupaziwa sauti, ili tujue namna ya kukabiliana nalo, kwa ajili ya kulinda maadili, afya na maisha ya baadaye ya mtoto,” anasema.
SHERIA YA MTOTO
Sheria ya Mtoto Sura Na. 13 ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019, inautaja wajibu na jukumu la mzazi katika kifungu cha 9 kifungu kidogo 3(a) kuwa ni kumlinda mtoto dhidi ya utelekezwaji, ubaguzi, vurugu, unyanyasaji, madhara ya kimwili na kiakili, na ukandamizaji.
Uchunguzi umebaini usalama wa watoto hao ni mdogo kutokana na kukosa uangalizi wa karibu. Watoto wamekuwa wakirandaranda ovyo mitaani na wakati mwingine kucheza katika maeneo yasiyo salama hali inayohatarisha afya ya akili na mwili kwa mtoto na maisha yake ya baadaye.
Katika sheria hiyo kifungu cha 9 (2), mzazi au mlezi anatakiwa kumpatia mtoto haki ya kupumzika na kuwa huru. kifungu hicho kikisomwa pamoja na namba 14 kuhusu adhabu ya ukiukwaji wake, mzazi atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani, atalipa faini isiyozidi Sh. milioni tano au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja.
Sheria ya Mtoto Sura Namba 13 ya Mwaka 2014 iliyofanyiwa marejeleo mwaka 2019 kuhusu amri ya malezi ya mahakama kwa faida ya mtoto kifungu namba 18(1) ikisomwa pamoja na (2) inasema:
“Mahakama inaweza, kutoa amri ya muda ya malezi kwa kumtoa mtoto katika mazingira yoyote yanayomdhuru au yanayoweza kumsababishia madhara na kuhamishia haki ya malezi kwa ofisa ustawi wa jamii endapo ofisa huyo ataomba kutolewa kwa amri hiyo.”
Vifungu hivyo vikisomwa pamoja na cha 7, vinaelekeza amri ya matunzo ya muda haitatolewa isipokuwa tu kama mtoto anapata madhara au kuna uwezekano wa kupata madhara kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 16 (a-q) cha sheria hii. Kifungu (o) kinasema mtoto atahitaji malezi na ulinzi endapo yuko katika mazingira yanayomhatarisha kimaadili au kimwili.
Wakati sheria hii ikisema hivyo, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwalaza watoto wao katika maboksi wakati wakipika au kuwa katika hatari ya kuungua moto, kugongwa na vyombo vya usafiri pamoja na kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Wengine kutokana na kukosa uangalizi, hurandaranda mitaani wakati wazazi wao wanaendelea na biashara hivyo kuwa katika hatari ya kupotea, kuibwa na hata kujihusisha katika makundi ya vitendo vya uhalifu.
KAULI ZA MAMALISHE
Mmoja wa mamalishe, Rehema Zuberi, mkazi wa Kata ya Ipuli, Manispaa ya Tabora, anasema kuambatana na mtoto wake si takwa lake, bali ni kutokana na kutelekezewa na mwenza wake.
Rehema mwenye mtoto wa kiume wa miaka minne, anasema baba wa mtoto huyo hatoi matumizi ambayo yangesaidia kuweka msaidizi nyumbani, hivyo analazimika kushinda naye kazini.
“Uwezo wa kumpeleka mtoto katika vituo vya kulea watoto kwa muda wa mchana sina, kulipa msaidizi sina, mtaji wenyewe ni wa shida, hivyo ninasubiri tu muda wa kuanza shule ufike aanze kushinda shuleni,” anasema.
Christina Andrea, mkazi wa Chemchem, mkoani hapa mwenye watoto watatu kati yao wawili ni wakubwa na mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minne, anasema analazimika kwenda naye mgahawani kwa kukosa mtu wa kumwachia.
“Si kwamba tunapenda kuja na watoto huku kwenye shughuli zetu, japo kwa kweli huku wanakuwa hawapati uangalizi mzuri kwa sababu tunakuwa na pilikapilika za kupika na kuhudumia wateja, hivyo wanakuwa katika mazingira ya hatari sana,” anasema.
Anitha Samweli, mkazi wa Ng’ambo Manispaa ya Tabora, mwenye watoto wawili wa kike, mmoja wa miaka mitatu na mwingine minne, anasema analazimika kwenda nao kusaidia kupika na kuhudumia wateja kwa sababu mwenza wake alifariki dunia na hana mtu wa kumsaidia.
Anasema anatambua watoto wanaoshinda katika mazingira ya mtaani wanajifunza mambo yasiyofaa ikiwamo lugha chafu, matendo mabaya na hivyo kuchangia uwezekano wa kuporomosha maadili yao.
WADAU WANENA
Mtaalam wa utengenezaji wa zana za kujifunzia na uchangamshi wa mtoto, ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Tuwaandae Pamoja kutoka Shirika la Tanzania Early Childhood Education and Care (TECEC) mkoani Mwanza, Ester Macha, anasema mtoto mwenye umri kuanzia miaka sifuri mpaka minane, ana uwezo wa kushika haraka kile anachofundishwa sambamba na anachokiona katika mazingira.
“Mtoto ukimwandaa vyema kwa kipindi hicho, utapata matokeo mazuri kwake, kwani atakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, kujiamini na kufanya vitu vyenye faida,” anasema.
Anasema kitendo cha watoto hao kukulia katika mazingira ya namna hiyo, kinawaweka hatarini si tu kwa maisha yao, bali hata tatizo la afya ya akili kutokana na kurundika mambo mengi na yaliyowazidi uwezo katika vichwa vyao.
“Katika maeneo hayo kuna watu wa tofauti, wenye matusi, utani usiofaa kwa wazazi wao, makundi ya aina tofauti anayokutana nayo wakati mzazi wake akiendelea na majukumu. “Hivi vyote vinaweka hatarini mustakabali mzima wa maisha ya mtoto, hivyo kuna haja ya suala hili kupatiwa ufumbuzi,” anasema Macha.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na kuhudumia jamii JIDA ya mjini Tabora, John Pinini, anasema kuna haja kwa serikali, wahisani na wadau kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, ili kuwaokoa watoto hao na mama zao.
“Kundi kubwa la watoto wanaoshinda na mama zao wanaopika mitaani haliko Tabora mjini pekee, bali ni maeneo tofauti nchini,” anasema.
Anasema watoto hujifunza mambo mengi mabaya na mengine yanayowazidi umri wao na kwamba, hata afya zao ni lazima ziwe hatarini kutokana na kushinda katika baridi, vumbi, upepo na wakati mwingine mvua.
Mkurugenzi wa Chuo cha Tabora Polytenics (TPC), Shaban Mrutu, anasema kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa watahakikisha wanafanya jitihada binafsi kuona namna ya kuwasaidia watoto hao na mama zao.
Serikali ina utaratibu wake katika kushughukia masuala mbalimbali, ila binafsi nina ahadi ya kutoa ushirikiano wangu wa hali na mali kuwasaidia.
“Niko tayari na milango ipo wazi kusaidia kwa namna yoyote ile kadri nitakavyoelekezwa na wahusika,” anasema.
VIONGOZI
Mmoja wa maofisa watendaji kata akiwamo, Salehe Mbuguma kutoka Kata ya Chemchem, anasema kuna uhitaji wa msaada wa kudhibiti hali hiyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Gongoni, Mzelela Kalamata, anasema mara kadhaa wamekuwa wakizuia kwa kushirikiana na maofisa afya kata, lakini wazazi wamekuwa wakidai kukosa namna ya kuwaacha nyumbani kutokana na kutokuwa na watu wa kuwaachia.
Naye Nasibu Lukeha, Mtendaji wa Kata ya Kanyenye, anasema kundi hilo la watoto ni muhimu kwa taifa, hivyo jamii inatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka kukabiliana nalo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Elias Kayandabila, amehidi kuhakikisha anawapanga wasaidizi wake hasa wa idara ya ustawi wa jamii kushughulikia tatizo hilo kwa kushirikiana na serikali, taasisi binafsi na wadau mbalimbali walio tayari, ili kupata ufumbuzi na kuliokoa kundi hilo.
Kayandabila anasema kundi hilo linaibuka na kuenea kwa kasi mitaani, kutokana na mama zao kutelekezwa na wenza wao, kuwa fukara, kukosa mitaji ya kuendeshea shughuli zao kwa uhakika na ufanisi, ili kuwezesha kukidhi mahitaji yao pamoja na familia zao.
Anasema watatafuta namna bora ya kuwapa elimu ya ujasiriamali, kuwahimiza kujiunga katika vikundi vinavyotambulika kisheria, ili kuweza kukopesheka na hatimaye kuwapa mikopo wakitimiza vigezo, ili kuwasaidia kujiongezea kipato na kumudu maisha.
Imeandaliwa na Benny Kingston (TABORA), Vitus Audax (MWANZA).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED