NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amewataka wadau wote wa takwimu rasmi kushirikiana na serikali katika kukokotoa viashiria vya maendeleo.
Amewataka kutathmini hatua zilizopigwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoisha mwaka 2025 na hatua zilizopigwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu yanayoisha mwaka 2030.
Chande alitoa rai hiyo wakati wa Mahafali ya 10 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) yaliyofanyika Dar es Salaam.
Alisema lengo la wadau wa takwimu rasmi liwe kuhakikisha takwimu zinakuwa rahisi kutumika katika kupanga mipango ya kukuza uchumi, kuboresha huduma za jamii, kutunza mazingira na kupunguza umasikini bila kuwaacha wengine nje.
“Ukuaji wa uchumi wa mmoja mmoja na ubora wa hali ya maisha na mazingira unatarijia mipango bora inayopimika kwa takwimu rasmi, hivyo katika mahafali haya. Nakipongeza chuo kwa kuzalisha wataalam mbalimbali katika tasnia pana ya takwimu rasmi na nawasihi kutimiza majukumu yenu kwa weledi ndani ya taifa, Afrika na duniani kote,” alisema.
Kuhusu matumizi ya kidigitali katika masuala ya takwimu, Chande alisema serikali tayari imeandaa mazingira kwa wananchi wake na wafanyabiashara kumudu mabadiliko ya kidijitali kwa kuweka anwani za makazi za kidijitali pamoja na maboresho ya teknolojia ya mawasiliano yanayorahisisha upatikani wa taarifa za sensa na tafiti ndogo katika ngazi ya vitongoji, mitaa na shehia.
Chande alisema kwa wadau wa sekta binafsi hususani rika la vijana, walio masomoni, wahitimu na walioko makazini, wanatakiwa kuwekeza zaidi katika sekta ya ubunifu wa mifumo ya biashara dijitali na kilimo cha kisasa.
Pia aliishukuru Kamisheni ya Uchumi Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), mabalozi, maofisa wakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, washirika wa maendeleo, wakurugenzi wakuu wa ofisi za taifa za takwimu za nchi wanachama wa chuo na wadau wengine wanaoshirikiana na chuo kwa kuwa kunawezesha kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kitaifa, kikanda na kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED