WAFANYAKAZI 25 wa kutoka nchini Marekani chini ya Mtandao wa Kimataifa wa Wafanyakazi wa Kujitolea (PEACECORPS) wameapishwa kwa ajili ya kuanza kazi hiyo nchini.
Akizungumza katika hafla fupi ya uapisho mapema wiki hii jijini Tanga, Balozi wa Marekani Nchini, Michael Battle, alisema wafanyakazi hao wapo tayari kuihudumia jamii ya Tanzania baada ya kupitia mafunzo ya wiki 12 ya kina.
Alisema mafunzo waliyopitia wafanyakazi hao ni lugha ya Kiswahili, utamaduni, ulinzi na usalama, afya na ujuzi mahsusi wa sekta katika kukabili na kutoa ujuzi kwa jamii.
Balozi alisema wafanyakazi hao wataishi na kufanyakazi kwa miaka miwili katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Njombe na Zanzibar wakifundisha masomo ya hisabati na sayansi, eneo la afya ya jamii, kilimo endelevu kinachohusisha ukuzaji wa ustahimilivu wa hali ya hewa katika shule za sekondari.
Aliwaeleza wafanyakazi hao kuziwezesha na kuziongoza jamii kufahamu vipaumbele na mahitaji yao, ili washirikiane kwa pamoja kutafuta ufumbuzi endelevu wa matatizo yao.
“Kazi mnayofanya hapa mkishirikiana na wafanyakazi wenzenu wa Kitanzania na majirani inaweza kubadilisha maisha. Muwe na ndoto kubwa, lakini kumbukeni kutokubaki na ndoto hiyo wenyewe,” alisema.
Alisema wafanyakazi hao wataungana na wenzao 3,200 katika kuenzi urithi ulioachwa na Mwalimu Julius Nyerere na Rais John Kennedy wa kujitoa kwa ajili ya amani na urafiki duniani tangu ilipoanza programu ilipoanza mwaka 1961.
Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania, Stephanie Joseph de Goes, alisema kinachofanya shirika hilo kuwa la kipekee ni mbinu yake ya kuleta maendeleo ya watu ikiwa ni kusimamia kwenye msingi wa ubia imara ulioanza zaidi ya miaka sitini iliyopita.
Aliishukuru Tanzania kwa msaada, ushirikiano wanaoutoa kwako, na kuwa imani walionayo kwao inawawezesha kuhudumu kikamilifu pande zote za nchi hiyo.
“Ni maendeleo yenye msingi wake kwa watu, yanayozingatia kujenga uhusiano mzuri na yanayopewa msukumo na mahitaji na matamanio ya jamii. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wabia wetu serikali ya Tanzania,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED