RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inadhamiria kuwa na umeme wa uhakika kutokana na kupanuka kwa shughuli za uchumi, miradi mikubwa ya maendeleo, ongezeko la hoteli za kitalii na kasi ya uwekezaji inayokua kila siku.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar, wakati akizungumza na ujumbe kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Rita Laraujinha, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Masuala ya Nje, Kanda ya Afrika baada ya kumtembelea.
Taarifa ya Idara ya Mawasiliano Ikulum Zanzibar ilimkariri Rais Mwinyi akisema kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikipokea megawati 100 za umeme kutoka Tanzania Bara kupitia waya za chini ya bahari ambao kwa sasa hautoshelezi.
Alisema kuna kila sababu ya kupata umeme mbadala na kufikiria kuwa na umeme wa jua, mawimbi au upepo na kuomba Umoja wa Ulaya (EU) kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kwenye eneo hilo.
Dk. Mwinyi alisema serikali inafikiria kuzisarifu taka kwaajili ya kupata umeme mbadala, hatua ambayo itadhibiti taka zinazozalishwa kila siku.
Kuhusu uwezeshaji wanawake kiuchumi, Rais Mwinyi alisema nia ya serikali ni kuwaongezea nguvu, uwezo na utaalamu wakulima wa mwani ambao asilimia 90 ni wanawake.
Kadhalika alisema kuliinua zao hilo pamoja na kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ili kuusarifu na kuzalisha bidhaa zinazotokana na zao hilo kwa kuziongezea thamani badala ya kuuza mwani kama malighafi.
Rais Mwinyi alisisitiza Umoja wa Ulaya kuiunga mkono Zanzibar katika azma yake ya kukuza uchumi kupitia sekta za kimkakati ikiwamo Uchumi wa Buluu na utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa serikali anayoiongoza.
Alisema hivi sasa Zanzibar inafanya utalii wa kisasa unaoshajihisha utalii wa kumbi za mikutano, utalii michezo na wa afya, ambapo awali ilijikita zaidi kuendesha utalii wa fukwe na maeneo ya urithi, ambao umezoeleka kwa muda mrefu.
Rais Mwinyi azikaribisha nchi za Umoja wa Ulaya, hususan sekta binafsi kuja Zanzibar kubaini fursa za uwekezaji zilioko, kwani kuna maeneo mengi hayajafikiwa hasa kwa sekta ya Uchumi wa Buluu kupitia utalii, bandari, mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini.
Kadhalika aligusia masuala ya jinsia na kueleza kuwa, serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha inaweka uwiano sawa kwa wananwake na wanaume kwa nyanja zote.
Aliuomba Umoja wa Ulaya kuunga mkono kwenye maeneo ya taaluma, kuwajengea uwezo wanawake kwa dhamira ya kuwainua kiuchumi.
Wakati huo huo, Rais Mwinyi ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano ulioko baina yao na misaada wanayoita kwa Tanzania hususani Zanzibar kwa sekta za jamii hasa kwa elimu, afya na ustawi wa jamii na kuwaomba kuendeleza misaada hiyo.
Rita Laraujinha, ameipongeza Zanzibar kwa ushirikiano wanaoutoa kwenye miradi inayosimamiwa na EU na kumwakikishia Rais Mwinyi kuwa wataendelea kuiunga mkono Zanzibar wa kuleta maendeleo hasa kwa masuala ya afya, elimu na Uchumi wa Buluu.
Alisema EU imerishwa na hali ya amani na utulivu ulioko Zanzibar na kwamba utaendelea wakati wote kuunga mkono juhudi za kuimarisha amani hiyo na kuona demokrasia inafuata mkondo wake kwaajili ya maendeleo ya nchi jamii kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED