Zahera: Namungo gari limewaka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:43 AM Sep 19 2024
 Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera

BAADA ya kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam dhidi ya Coastal Union, Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera, amesema tayari wachezaji wake wameshaanza kuyashika vyema mafunzo wanayopatiwa.

Namungo ilipata ushindi wa mabao 2-0, ukiwa ni wa kwanza kwenye ligi, tena ikiwa ugenini, baada ya kupoteza mechi zake zote tatu ilizocheza awali, ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Tabora United, 2-0 dhidi ya Fountain Gate, ikiwa nyumbani, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi na bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, mkoani Manyara.

"Tatizo letu kubwa haikuwa kucheza vibaya, ilikuwa pale mbele jinsi ya kumalizia, na hilo ndiyo tumelifanyia kazi na sasa limeanza kutoa matunda. Coastal si timu ya mzaha, ni timu ngumu iliyopata michezo migumu ikiwamo ya kimataifa, Kombe la Shirikisho, kwa hiyo kushinda kwetu mabao 2-0, ni mwanzo mzuri na sasa hata wachezaji wetu kisaikolojia watakuwa vizuri, natumai tutaendelea kufanya vizuri," alisema Zahera.

Coastal inatumia Uwanja wa Azam Complex, kutokana na Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga kuwa katika matengenezo.

Yalikuwa ni mabao ya Rith Nkoli dakika ya 37 na Pius Buswita dakika ya 45 yaliyoifanya timu hiyo kupata ushindi na kusogea hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kipigo hicho kimeifanya Coastal Union kushuka hadi nafasi ya 14 ya msimamo ikiwa na pointi moja tu baada ya kucheza michezo mitatu, haijapata ushindi wowote mpaka sasa, ikitoa sare moja na kupoteza miwili.