ZIKIWA na kumbukumbu ya kuishia katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa vigogo wa soka nchini, Yanga na Simba watakutana katika mechi ya dabi itakayochezwa leo kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ni ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na wenyeji wa mchezo huo, Yanga wataingia dimbani na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5-1, ambayo yalifungwa na Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili.
Bao pekee la Simba katika mchezo huo lilifungwa na Kibu Denis.
Katika rekodi zetu kuanzia mwaka 2010, zinaonyesha Aprili timu hizo zimekutana mara nne, Simba walifanikiwa kushinda mara mbili na michezo mingine miwili iliyobakia ilimalizika kwa matokeo ya sare.
Aprili 18, 2010 Simba alishinda mabao 4 -3, na mabao yake yalifungwa na Uhuru Suleiman dakika 3, Mussa Mgosi (dk 53 na dk 74), Hillary Echesa (dakika za nyongeza) huku kwa upande wa Yanga yalipachikwa na Athumani Iddi 'Chuji' dakika 30 na Jerry Tegete aliyefunga mawili (dakika 69 na 89).
Mechi ya kwanza ya Aprili 19, 2014 iliisha kwa sare ya bao 1-1, Simba walitangulia kupata bao kupitia Haruna Chanongo na dakika nne kabla ya mechi kumalizika, Yanga walisawazisha kupitia Simon Msuva.
Msimu wa 2017/18 mechi iliyochezwa Aprili 20, Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kupitia Erasto Nyoni na timu hizo ziliporudiana mchezo ulimalizika kwa suluhu.
Mchezo wa mwisho uliochezwa Aprili 16, mwaka jana, Simba iliondoka na pointi tatu baada ya kushinda mabao 2-0, shukrani beki Henock Inonga akipachika bao la mapema dakika ya kwanza na lingine lilifungwa na Kibu Denis dakika 32.
Mechi ya leo haitakuwa ya kinyonge kutokana na rekodi za timu hizo hivi karibuni, mechi tano za mwisho walizokutana Simba ilishinda mbili na Yanga mara moja, wakitoka sare mara mbili.
Yanga inashuka dimbani ikiwa na safu imara ya ushambuliaji inayoongozwa na Stephane Aziz Ki ambaye ametikisa nyavu mara 14 pamoja na Nzengeli aliyefunga magoli tisa wakati Simba inamtegemea Clatous Chama mwenye magoli saba sawa Mrundi Saido Ntibazonkiza.
Yanga na Simba, zote zipo katika mbio za ubingwa, Yanga wakiongoza kwenye msimamo baada ya kujikusanyia pointi 55 na Simba iliyoko katika nafasi ya tatu na pointi zake 46 ingawa imecheza mechi tatu pungufu ya Azam yenye pointi 51.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemtaja mwamuzi, Ahmed Arajiga kutoka Manyara atakuwa mwamuzi wa kati na atasaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga, Kassim Mpanga (Dar es Salaam) na Tatu Malogo (Tanga).
Akizungumza jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema hii ni mechi kubwa sana Afrika Mashariki na leo itakuwa ni sehemu ya mchezo mkubwa kwa Afrika.
Gamondi alisema wamejiandaa vizuri kama kawaida, wachezaji wake wana morali nzuri na wapo tayari kukabiliana na mpinzani wao, Simba katika mchezo wa leo.
“Kesho (leo) ni mechi nyingine na mipango yake ni mingine, huu mchezo ni tofauti na ule uliopita, tutacheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha tunafanikiwa kupata matokeo chanya,” alisema Gamondi.
Beki wa Yanga, Dickson Job, alisema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kwa ajili ya kutafuta matokeo chanya mbele ya mpinzani wao.
“Simba ni timu nzuri na hautakuwa mchezo rahisi, mchezo utakuwa mgumu, kikubwa tunahitaji pointi tatu, hatuchezi kwa presha kubwa wala matokeo ya kutaka kushinda mabao mengi kikubwa ni alama muhimu,” alisema Job.
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema maandalizi yanaenda vizuri na siku zote hakuna mechi rahisi ya dabi na anawaheshimu Yanga.
“Hatuna presha kabisa, mechi ya dabi ni tofauti kabisa na michezo mingine, tumefanya maandalizi mazuri kukabiliana na Yanga, Kocha Abdelhak (Benchikha), anaumia sana pale tunapotengeneza nafasi na haziwi mabao, tumeliangalia na kufanyia kazi, nafasi zinazopatikana ziwe mabao.
Mbio za ubingwa zipo wazi na mchezo wa kesho (leo), ndio unatoa taswira ya nani kubwa bingwa, tukihitaji ubingwa lazima tushinde mechi ya kesho (leo) dhidi ya Yanga,” alisema Matola.
Nahodha Msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe, alisema maandalizi yameenda vizuri na wachezaji wana morali kubwa kwa ajili ya mchezo wa leo huku benchi la ufundi likipata muda mzuri wa kuandaa timu yake.
Kapombe alisema wapo tayari kufuata maelekezo waliyopewa na kila mmoja kufanya jukumu lake kwa ajili ya kutafuta pointi tatu muhimu.
"Kwa sasa hatufikirii mechi iliyopita, tumefungua ukurasa mpya na hii mechi ni aina nyingine, tumekuwa na mikakati mipya kuhakikisha tunavuna pointi tatu,” alisema Kapombe.
Aliongeza mechi ya leo itakuwa ni hatima ya malengo ya kusaka tiketi yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na anaimani hadi sasa bado hajajulikana bingwa hadi mwisho wa msimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED