Mwinjilisti Ezekiel Odero atoa million 10 kuishika mkono Timu ya Pamba

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:18 PM Jul 17 2024
MWINJILIST Ezekiel Odero wa Kanisa la Newlife Prayer Center and Church kutoka Mombasa nchini Kenya (kushoto) baada ya kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda Sh. milioni 10 kama msaada kwa timu ya Pamba.
Picha: Neema Emmanuel
MWINJILIST Ezekiel Odero wa Kanisa la Newlife Prayer Center and Church kutoka Mombasa nchini Kenya (kushoto) baada ya kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda Sh. milioni 10 kama msaada kwa timu ya Pamba.

MWINJILIST Ezekiel Odero wa Kanisa la Newlife Prayer Center and Church kutoka Mombasa nchini Kenya amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Sh.million 10 kwa ajili ya kuifadhili timu inayowakilisha mkoa huo ya Pamba huku akitoa ahadi ya kununua mipira mitatu na jezi pea mbili kwa kila mchezaji.

Akizungumza mara baada ya kukagua na kuubariki  Uwanja wa CCM Kirumba ambao atautumia kufanya mkutano mkubwa wa Injili Julai 24 hadi 28  mwaka huu. Alisema amewiwa kuwawezesha vijana hao ili waweze kufikia malengo yao ya kisoka na kurejesha furaha kwa wananchi iliyopotea takribani miaka 23 mara baada ya timu hiyo kushuka daraja.

"Ninaomba kama kunaweza kupatikana duka zuri linalouza unifomu ( jezi ) kati ya leo (Jana) na wiki ijayo tunaweza kupanga na kuzilipia hizo jezi pea mbili na mipira mitatu ambazo zitasaidia timu kucheze vizuri,timu inahitaji jezi nzuri zilizodizainiwa vyema zikiwa na majina ya wachezaji " alieleza Ezekiel.

Aliongeza kuwa Mwenyezi Mungu akiwapa  neema mara baada ya mkutano watapita kuwasalimia wachezaji na watachangia kile ambacho Mungu amewawezesha kwa sababu Mungu uweka watu uongozini kwa ajili ya wale wanaoongozwa waishi maisha mazuri kama wale waliouongozini hivyo neema ambayo tutajaliwa itawasaidia na wao pia.

"Mimi kipindi cha nyuma nilikuwa mchezaji na nilicheza namba 11 lakini kwa sasa siwezi tena kucheza lakini naweza kuwawezesha vijana na kuwashika mkono " anaeleza.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,  anaeleza kuwa moja ya kilio cha wananchi ni kuona timu yao inasimamiwa vyema ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya ligi kuu hivyo wametumia takribani Sh. million 300 katika usajili kuhakikisha tunakuwa na timu bora.

Alisema mwezi wa nane watafanya tamasha kubwa ili kufanikisha ununuzi wa basi ambalo linagharimu Sh.million 450 ambapo wao wameshakusanya million 250  na wanaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali ili waweze kuwashika mkono na wamewaomba baadhi ya viongozi wizarani wasaidie kufanya hamasa kwa wadau ili kufanikisha ununuzi wa gari hilo.

" Na sisi tunaendelea kuhamasisha tumepata wadau ambao wametudhamini takribani Sh. million 400 za uendeshaji wa timu, kwahiyo jumla Kuu ya uendeshaji wa timu ni zaidi ya Sh.billion 1.5 kwa msimu kwa mchango huu naamini utafungua njia kwa wadau wengine kwa sababu uendeshaji wa timu ni mkubwa.