WAKATI kukiwa na taarifa ya Mwekezaji wa Klabu ya Simba na Rais wa Heshima, Mohamed Dewji kuwaondoa wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi wa upande wake ndani ya klabu ya Simba, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez anatajwa kurejeshwa na kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa bodi hiyo kwa muda.
Inaelezwa, Barbara atasimamia upatikanaji wa kocha mpya na kusaidiana na wateule wengine kufanya usajili wa maana ndani ya klabu hiyo kabla ya kurejea kwenye nafasi yake ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema uamuzi huo umefikiwa ili kuirejesha Simba kwenye makali yake ikikumbukwa chini ya Barbara ilikuwa ikifanya vizuri ndani na nje ya nchi huku kiongozi huyo akiwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa watu wa ndani ya klabu hiyo alikiri kutokea kwa mabadiliko hayo yenye lengo ya kuipa makali Simba msimu ujao.
"Ni kweli hilo limetokea, matokeo ya msimu huu ndio chanzo, imeonekana baadhi ya watu ndani ya uongozi hawawajibiki, tunakoelekea mwanga umeanza kuonekana ndani ya Simba, usajili utasimamiwa na watu makini na wenye uzoefu," alisema mtoa taarifa hiyo.
Alisema kila kitu kikiwa tayari wana simba watataarifiwa kufahamu nini kinaendelea na maamuzi yaliyochukuliwa.
"Simba ya msimu ujao itakuwa ya tofauti sana na msimu huu, heshima ya klabu itaanza kurudi na kuendelea kutamba kwenye soka la ndani na nje," alisema mtoa taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, mmoja wa wajumbe walioondolewa na Dewji, Rashid Shangazi alikiri kubwaga manyanga kwenye nafasi hiyo.
Shangazi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mlalo, amesema jana kuwa, amefanya maamuzi hayo kama sehemu ya uwajibikaji kwa ajili ya kutengeneza utawala bora, huku akiwasihi wenzake waliofanya kama yeye kuwapa ushirikiano watakaoteuliwa.
"Nimejiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji, mwenendo wa timu haukuwa mzuri, wanachama wenzangu na mashabiki wana manung'uniko, miongozi mwa malalamiko yao ni kuona bodi na menejimenti tulishindwa kutekeleza wajibu wetu vizuri, wakati mwingine unawajibika kwa ajili ya kutengeneza utawala bora na wengine waje kusukuma gurudumu," alisema mjumbe huyo.
Hata hivyo alikanusha taarifa kuwa wameshinikizwa kujiuluzu, badala yake kila mmoja amefanya hivyo kwa manufaa ya klabu.
"Ukweli ni kwamba hatukulazimishwa au kutakiwa kujiuzulu na mwekezaji, unawezaje kushinikizwa?, Ni mambo tu ya kwenye mitandao, kila mmoja ameteuliwa kwa wakati wake, ila kuna suala la kujitathmini, inawezekana tu kuwa jana (juzi) ilikuwa ni siku ya mwisho ya kujiuzulu, kwa taarifa tu ni kwamba mimi niliandika barua wiki moja iliyopita, wengine walishajiuluzu mwezi mmoja uliopita ni suala tu la uwajibikaji na kujitathmini si suala geni, ni namna tu ya kuipa taasisi nafasi ya kupumua," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umoja na mshikamano uendelee huku akiwasihi wenzake wanaoondoka kuwapa ushirikiano watakaokuja ili kutengeneza Simba yenye mafanikio ndani na nje ya uwanja.
"Umoja na mshikamano ndiyo suala la msingi, niwasihi tu Wanasimba hiki ni kipindi cha mpito, ni vyema tukawa pamoja, tukashirikiana, tumeondoka ili kumpa mwekezaji wetu nafasi ya kuunda upya safu yake na kuipa ushirikiano kuanzia nje ya uwanja, tukifika ndani hata vijana wetu ambao tutakuwa tumewasajili watajua dhana ya nguvu moja ipo, watafanya vizuri," alisema.
Awali, taarifa zinasema Mo, aliwapigia simu akiwataka waandike barua za kujiuzulu lengo likiwa kuunda safu mpya ya uongozi kabla ya kuanza mchakato wa usajili.
Taarifa za awali zinasema kuwa baadhi walikuwa wamejiuzulu na wengine waligoma, lakini baadaye wote walikubali kujiuzulu akiwemo mwenyekiti wa bodi hiyo Salim Abdallah 'Try Again'.
Mbali yao hao wengine ni pamoja na Raphael Chageni, Hamza Johari, na Zulfikar Chandoo.
Kwa misimu mitatu, Simba imekuwa haifanyi vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, na msimu huu imeshindwa kabisa kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo msimu ujao itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza Ligi Kuu ikishika nafasi ya tatu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED