KIUNGO mkabaji mpya wa Yanga, Aziz Andambwile, amesema ilikuwa ni ndoto yake kujiunga na klabu hiyo, hivyo kitu kikubwa zaidi kwake ni kupambana ili kupata namba katika timu hiyo yenye wachezaji wakubwa na mahiri Afrika.
Akizungumza akiwa kambini Kigamboni, Dar es Salaam, alisema hata baba yake mzazi baada ya kusikia habari za kusajiliwa Jangwani alimuusia kuwa ajichunge na kwenda kupambania namba na si kitu kingine.
Andambwile, mmoja wa viungo wakabaji wanaokuja juu kwa sasa nchini, amesajiliwa hivi karibuni na Yanga, akitokea Singida Fountain Gate.
"Nimepata mapokezi makubwa kutoka kwa wenzangu, safari yangu ya soka ni ndefu sana hadi hapa nilipofika na kwa sababu nimepata nafasi hii adimu ya kufika Yanga, inabidi nipambane ili kuipata namba, kwa hiyo niko tayari kwa hilo, hata baba yangu mzee Andabwile baada ya kusikia nimesaini Jangwani, alinipa nasaha zake, akaniambia unakwenda kukutana na watu wapya, changamoto mpya, hivyo kazi kubwa ni kujichunga na kupambania nafasi mwanangu," alisema.
Alisema kuwa anajisikia furaha sana kujiunga na timu kama Yanga ambayo kwa sasa ina mafanikio makubwa na wachezaji wakubwa, huku yeye mwenyewe akitarajiwa kuwa atakuwa mmoja wa watu wenye mafanikio ya hao aliowakuta.
"Kila mmoja ana ndoto kucheza timu yenye mafanikio makubwa kama Yanga, na mimi pia baadaye nitakuwa ni mmoja kati wachezaji wenye mafanikio kwa mataji," alisema mchezaji huyo ambaye kabla ya kujiunga na kikosi cha Fountain Gate, aliichezea Mbeya City.
Alionyesha furaha yake alipowakuta wachezaji wenzake ambao amezoeana nao kabla hata ya kujiunga na kikosi hicho.
"Nimekutana na rafiki zangu hapa, Kibwana Shomari na Dickson Job tunafahamiana kabla sijafika na wao ndiyo wanaonifanya niwe kama mzoefu hapa, nimefurahi sana," alisema.
Aliwaahidi wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa watamuona Andambwile yule yule waliokuwa wakimuona akiwa Mbeya City na baadaye Singida Fountain Gate.
Hata hivyo kiungo huyo atakuwa na changamoto kubwa kwani atakutana na Khalid Aucho, mmoja wa viungo wakabaji bora nchini, na Mudathir Yahaya, ambaye mbali na kukaba, lakini ana uwezo mkubwa wa kupachika mabao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED