Masomo hisabati, sayansi hadi kieleweke

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 01:13 PM Feb 22 2025
Mratibu wa Mafunzo Kituo cha Shule ya Sekondari Bagamoyo, Winchslaus Balige akizungumza katika mafunzo hayo
Picha: Grace Mwakalinga
Mratibu wa Mafunzo Kituo cha Shule ya Sekondari Bagamoyo, Winchslaus Balige akizungumza katika mafunzo hayo

SERIKALI, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini, kwa kuanzisha mafunzo endelevu kwa walimu wa masomo hayo.

Hatua hiyo imebainishwa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Jimmy Nkwamu, wakati akifungua mafunzo ya siku tano, kwa walimu shule za sekondari wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Nkwamu amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa sayansi, kwa kuwa walimu watakaopata mafunzo watatumia mbinu walizojifunza kuwahamasisha na kuwafundisha wanafunzi kwa ufanisi zaidi. 

“Tunatarajia kuona ongezeko la wataalamu wa sayansi nchini, kwani walimu watakuwa na ujuzi wa kufundisha kwa vitendo na kutumia zana zinazopatikana kulingana na mazingira yao. Hii itasaidia wanafunzi wengi kuvutiwa na masomo haya badala ya kuyaogopa kwa kudhani ni magumu,” amesema Nkwamu.

Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani, Jimmy Nkwamu akizungumza na walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa walimu hao yanayofanyika wilayani Bagamoyo katika Shule ya Sekondari Bagamoyo
Kwa mujibu wa Nkwamu, kupima ubora wa mafunzo hayo, maofisa elimu wa mikoa nchini, wamepewa jukumu la kufuatilia na kuhakikisha kuwa walimu waliopata mafunzo wanatumia maarifa na mbinu mpya kufundishia wanafunzi, vilevile matokeo ya mitihani yatachukuliwa kama kipimo cha ufanisi wa mafunzo hayo kwa walimu.

Mratibu wa mafunzo hayo, Winchslaus Balige katika Kituo cha Shule ya Sekondari Bagamoyo, amesema jumla ya walimu 1,071 kutoka mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro wanashiriki mafunzo hayo. 

Amefafanua kuwa kupitia Mradi wa Kuimarisha  Elimu ya Shule za Sekondari (SEQUIP), walimu wanajengewa uwezo wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama nyenzo muhimu ya kufundishia, pamoja na mbinu za kubuni na kutumia zana za kufundishia kulingana na mazingira yao. 

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha walimu wa Sayansi na Hisabati wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayohimiza matumizi ya mbinu za kisasa za kufundishia ili kuendana na mahitaji ya karne ya 21,” amesema Balige. 

Mwenyekiti wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Dk. Emmanuel Sulungu ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema matarajio makubwa ya mafunzo hayo ni kuongeza ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

“Tunahimiza walimu kutumia mbinu mpya wanazopata katika mafunzo hayo, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopenda na kufaulu masomo ya sayansi na hisabati, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiogopwa na wanafunzi,” amesema Dk. Sulungu. 

Miongoni mwa walimu wanaoshiriki mafunzo hayo walieleza matarajio yao akiwamo, Esther Mianga, kutoka Shule ya Sekondari Makumbusho, Dar es Salaam, amesema anatarajia kupata mbinu mpya ambazo zitamsaidia kuboresha ufundishaji wake. 

Mwalimu Mdalahela Raina, anayefundisha somo la Hisabati katika Shule ya Sekondari Mbasa, Ifakara, Morogoro, amesema kupitia mafunzo hayo, atajifunza matumizi ya zana za kufundishia na Tehama ili kuboresha ufundishaji wake.

00000