WAKATI CCM imewahi kuteua wagombea badala ya kusubiri Julai kama ilivyozoeleka kwa miaka mingi, vyama vingine hasa vya upinzani vina cha kujifunza.
CCM imeondoka Dodoma na majina ya wagombea wake wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar. Ni kipindi ambacho CHADEMA wanaendelea kujipanga wampe nani uongozi wa chama kati ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Tundu Lissu.Jana CHADEMA walitarajiwa kuwapata viongozi wakuu wa chama kwenye uchaguzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
CCM imempitisha Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, wakati kwa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi amepitishwa kuwania muhula wa pili.
Baadhi ya wachambuzi wanasema ni kama kutimiza utaratibu ambao ni lazima iwe hivyo, kwa kuwa CCM ina kawaida ya kumpa mgombea urais miaka 10 ya uongozi bila kubadilishwa au kuteua mwingine kama inavyoelekezwa na katiba yake.
Kwa upande wa CHADEMA wana cha kujifunza kuwa mwaka wa uchaguzi mkuu siyo muda wa kufanya uchaguzi wa viongozi wakuu na wengine ndani ya chama badala yake wabadilishe taratibu na kuanza kujiweka kwenye kutumia mwaka wa uchaguzi mkuu kuweka na kujiimarisha na kuvuta wanachama na wapenzi wengi ili kutoa upinzani kwa chama tawala.
Mwaka 2019 Mbowe alichaguliwa tena katika nafasi ya uenyekiti dhidi ya mpinzani wake Cecil Mwambe, katika matokeo yaliyotangazwa Desemba 19, 2019.
Ukiangalia kitakachoendelea CCM ni kuwavuta na kuwaonyesha wananchi kuwa hawayumbi na kuelekea uchaguzi mkuu wako tayari ili kwa CHADEMA kinachojiri ni mnyukano wa kutafuta viongozi wa chama hicho taifa, ndipo viongozi watakaochaguliwa wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Inawezekana kuwa ni kuchelewa kwa upande mmoja, lakini inaweza kuwa ni kuendeleza siasa za mazoea wakati CCM wanaonyesha kubadilika.
Historia ya uteuzi wa wagombea urais ndani ya CCM inaonyesha kuwa kazi hiyo inafanyika Julai kila mwaka wa uchaguzi mkuu, lakini safari hii wamewahi na kuifanya mwanzoni mwa mwaka.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema huenda wamejihami ili kujiepusha na upinzani ndani ya chama kama ilivyotokea 2020.
Uchaguzi mkuu wa 2020, ulishuhudia baadhi ya wana CCM akiwamo Benard Membe (marehemu) wakitangaza nia ya kugombea urais licha ya utaratibu wa chama wa kuachiana miaka 10 bila upinzani wa ndani.
Hatua hiyo ilisababisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa awamu ya tano na mbunge wa Mtama, kufukuzwa uanachama wa CCM huku ndoto yake ya kugombea urais kupitia chama hicho ikitoweshwa.
Ilikuwa ni baada ya kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili, Udhibiti na Nidhamu ya CCM mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine, alituhumiwa kwa utovu wa nidhamu, hatua zilizochukuliwa mwanzoni mwa mwaka huo.
Membe alijiunga na Chama cha ACT Wazalendo na kupewa nafasi ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo wa 2020, huku mpinzani wake John Magufulu, akimshinda kwa kiwango kikubwa.
Pengine ni katika kuwahi kuondoa migogoro na makundi ndani ya chama, CCM ikawahi kuwathibitisha na kuwateua wagombea wake wa urais mwaka huu.
Kila masika yana mbu wake hata katika sakata hilo la Membe, baadhi ya wanachama wakongwe kama Sophia Simba, Jessica Msambatavangu na Omary Madenge walitimuliwa ndani ya chama kabla ya kurejeshewa uanachama baadaye.
Licha ya kwamba CCM imekuwa mstari wa mbele kuzuia kampeni za mapema na kutia nia ya kugombea urais. Baadhi ya wanachama walidaiwa kuonyesha nia ya kujitosa katika kinyang’anyiro.
Utauzi huo wa CCM ni kama umewapa watiania wa kificho muda wa kujitafakari na kujipanga mapema kama watakimbilia upinzani au watabaki ndani ya chama na kusubiri uchaguzi mkuu mwingine, tofauti na miaka ya nyuma walitimkia upinzani baada ya kukosa kura za kutosha katika uteuzi wa awali.
Wapo baadhi ya makada kama Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa (marehemu), ambaye alihamia CHADEMA mwaka 2015 na kupewa nafasi ya kuwania urais, kadhalika Membe naye baada ya kufukuzwa CCM.
Uteuzi huo wa Dodoma uwe king’ora cha kuiamsha CHADEMA na upinzani kwa ujumla kuwa hakuna wakati wa kupoteza kama wanataka kuingia katika uchaguzi mkuu na kushindana bila kuwa na ‘figisu.’
Lakini pia vyama vya siasa visiishi kwa kukariri muda na matukio, bali linalowezekana leo lisingoje kesho, hasa masuala yanayohusu uchaguzi kwa ujumla.
Vyama vya upinzani vingejifunza namna bora ya kukabiliana na makundi yanayoongeza mgawanyiko katika vyama na kusababisha vikose nguvu ya kuikabili CCM.
La muhimu zaidi wakati huu ni kuwaunga mkono na kuwapa nguvu wagombea wanaokubalika badala ya kila chama cha upinzani kusimamisha mwanachama wake hata kama hafahamiki.
Si vibaya kujifunza kwa chama kinachoonekana kufanya vizuri kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa demokrasia, ikiwamo kuiga yale ambayo yamefanywa na ACT Wazalendo na CCM.
UTEUZI WA NCHIMBI
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, umeandika historia baada ya kumteua mgombea mwenza urais, Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye atamrithi Dk. Philip Mpango, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Dk. Nchimbi anaonekana kuwa mpole, mnyenyekevu na msikivu asiye na siasa za majitaka anayejali na kuwa kiungo muhimu katika kufanikisha mustakabali wa R4 za Rais Samia.
Mwanasiasa huyo mwenye msimamo usioyumba, wakati wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, baada ya kusajiliwa mapingamizi mengi dhidi ya wapinzani, aliomba Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuangalia uwezekano wa kuachana na mapingamizi yasiyo na mashiko ili kupiga kura na kupanua demokrasia.
Kadhalika, Nchimbi ambaye ni mwanadiplomasia, sio mtu mwenye papara, kiburi cha uzima wala si mfuasi wa siasa za jino kwa jino au ukipigwa ni lazima urudishie.
Ana imani kwamba upinzani si uadui kama ambavyo Rais Samia amekuwa akisema wapinzani ni sehemu ya Watanzania na washauri ikiwataka wakosoe serikali kwa hoja na kupendekeza ufumbuzi wa hoja zao ili kuleta maendeleo.
Dk. Nchimbi anaweza kuchukuliwa kama kiunganishi cha CCM, vyama vya upinzani, serikali na wananchi, pale ambapo kuna jambo haliko sawa anaweza kulisawazisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED