Utaratibu ajira watihimu la VII waondolewa JWTZ

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:22 AM May 21 2024
Vijana wa JWTZ wakiwa mafunzoni.
Picha: Mtandaoni
Vijana wa JWTZ wakiwa mafunzoni.

UTARATIBU wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba kwenye Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) umeondolewa, serikali imeliarifu Bunge.

Naibu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, aliyasema hayo jana bungeni  alipojibu swali la Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.

Mbunge huyo alitaka kauli ya serikali juu ya mpango wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Pinda alisema JWTZ huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara. 

"Utaratibu wa kuandikisha jeshini askari wapya umefafanuliwa kwenye Kanuni ya 5 ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala). Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba," alisema.

 Kuhusu kuongeza idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne, Naibu Waziri Pinda alisema hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika. 

 "Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa kibajeti, nafasi hizi hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi," alisema. 

 Akiuliza swali ya nyongeza, Mbunge Cherehani alisema hakuna uwiano wa vijana wanaoingia katika mafunzo na wale wanaoajiriwa na kuhoji mkakati wa muda mfupi na muda mrefu wa serikali kuhakikisha vijana wanaajiriwa.

Pia alisema vijana hao wanapokuwa katika mafunzo kumekuwa na changamoto ya miundombinu na kuhoji mkakati wa serikali kukabiliana na tatizo la miundombinu.

Naibu Waziri Pinda, akijibu maswali hayo, alisema suala la ajira linategemea nafasi zinazotolewa na serikali.

Kuhusu miundombinu, Pinda alisema serikali imekuwa ikiviangalia vyombo vya ulinzi na usalama kwa upekee na hivyo hakuna uhakika wa ukosefu wa vifaa na miundombinu ya mafunzo katika kambi za jeshi.

Alisema serikali imeweka miundombinu wezeshi kwa vijana ili kupata mafunzo wezeshi yatakayowasaidia kumaliza mafunzo yao.