Ziara ya Makonda yafagia vigogo watano

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 07:50 AM Jun 01 2024
news
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameagiza kuhamishwa kazi kwa watumishi watano walioko kwenye idara na vitengo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kutokana na kukaa muda mrefu na kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo.

Kadhalika, Makonda ameagiza kushushwa vyeo Ofisa Elimu Msingi, Hussein Bakari na Ofisa Elimu wa Sekondari, Yusuph Mange.

Makonda alifikia hatua hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi katika viwanja vya Kilombero jijini Arusha huku akisema kuna miradi mingi imekwamishwa pasipo sababu za msingi na hawako tayari kuwavumilia watendaji wazembe.

Aidha, Makonda alimtaka Mkurugenzi wa Jiji, Mhandisi Juma Hamsini, kueleza watumishi ambao wanakwamisha miradi ya maendeleo akamjulisha waliofanya kazi kwa zaidi ya miaka mitano katika kituo kimoja cha kazi wahamishwe.

“Wakuu wa idara ambao ni zaidi ya miaka mitano niwatakie kila la heri na utaratibu wenu utaandaliwa na Katibu Tawala wa Mkoa. Si kwamba nawachukia, hiki kibarua si chetu ni cha wananchi na wale ambao wa msingi na sekondari mnapotoka katika huu uwanja si wakuu wa idara na kama mna magari myakabidhi kwa mkurugenzi,” alisema.

Mkonda alisema wafanyakazi waliobaki sasa ni wakati wa kufunga mkanda watapitia kila mkuu wa idara kuangalia utendaji wa kazi. Alisema  ili kuwajibika kwa Pamoja, kila mmoja anatakiwa kusimama katika nafasi yake ikiwamo kutatua kero za wananchi.

Aidha, Makonda alisema kuna fedha ambazo zimeshindikana kutumika matokeo yake wanafunzi wanakosa matundu ya choo, madarasa na mabwalo.

“Si kwa sababu fedha hakuna ni mtu mmoja ameamua kukaa kimya, hii ndio tafsiri yake. Hatuwezi  kufanya kazi kwa aina hii. Ujenzi  wa shule ya ghorofa na matundu ya choo ifikapo Juni inatakiwa iwe imekamilika. Zabuni  ilikosa mzabuni na kurudiwa kutangazwa upya mara ya pili na thamni yake ni Sh. milioni 240. Fedha  zipo mradi haujaanza,” alibainisha.  

Alisema maboresho ya ujenzi wa Shule ya msingi Imara yanayogharimu Sh. milioni 16, mradi haujaanza kutekelezwa na idara ya elimu ya msingi haijawasilisha vinavyotakiwa idara ya ununuzi.

“Sh. milioni 25 ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi Kijenge hakuna kilichofanyika kwa sababu idara ya msingi haijapeleka mahitaji kwenye idara ya ununuzi. Ukarabati wa madarasa manne katika shule za msingi Matebesi, Nanenane, Ngarenaro na  Makumbusho, yote hii miradi haijakamilika na fedha zipo lakini hazijatumika,” alisema.

Makonda, baada ya kusema hayo, aliwaita maofisa elimu hao huku akieleza maabara hazijajengwa, ujenzi wa bwalo lenye thamani ya Sh. milioni 80 hakuna kilichoendelea na miradi mingi imekwama na kusababisha changamoto kwa wanafunzi.

“Kuna watu wanalipwa mishahara tena ni mikubwa na watoto wanaamini hatuna fedha kumbe ipo ila ni uzembe wa watu kutowasilisha mahitaji kwa idara ya ununuzi. Kila  sehemu hakuna palipoanza kisa idara ya elimu haijawasilisha taarifa.

“Nyie si ndio mnawasimamia watoto wetu? Kuanzia  leo (juzi) nyie si wakuu wa idara zenu. Andikeni barua wenyewe mmwambie Katibu Mkuu kuwa mkuu wa mkoa ametuambia kutokana na uzembe na kushindwa kusimamia idara zetu kumesababisha watoto wa Jiji la Arusha kukosa matundu, madarasa na stahiki zao zote ikiwamo maabara hatufai kuwa wakuu wa idara. Tumeelewana … tumemalizana,” alisema.

Makonda alisema kwa cheo chao hawalipwi mshahara peke yake wanapewa na fedha za mawasiliano, usafiri na posho yao hailingani na mwalimu wa kawaida.

“Wanakula pakubwa kuliko wanachokifanya. Nilishasema  nitawapiga spana mpaka wanyoke. Mliponikaribisha nilisema kila mtumishi akae na kuenea katika kiti chake. Leo (juzi) tunamsikia mkuu wa kitengo cha ununuzi anaeleza hii wiki wanakimbizana ,ina maana kulikuwa na uzembe,” alisema.