Wiki ya Sheria yapiga hodi shuleni Kibasila

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 10:59 AM Jan 28 2025
Wakili wa kujitegemea, Dk. Aloys Rugazia, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika viwanja vya shule ya sekondari Kibasila, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam, kuhusiana na maandalizi ya kutoa elimu ya sheria katika kuadhimisha Siku ya
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakili wa kujitegemea, Dk. Aloys Rugazia, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika viwanja vya shule ya sekondari Kibasila, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam, kuhusiana na maandalizi ya kutoa elimu ya sheria katika kuadhimisha Siku ya

KAMPUNI ya Sheria ya Afrifa Legal Consultant, inatarajia kutoa mafunzo ya msingi wa haki kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kibasila, iliyoko Temeke, jijini Dar es Salaam, kuadhimisha wiki ya sheria.

Kadhalika, wananchi wametakiwa kufika eneo hilo, ili kupata huduma za kisheria bure na kujua haki zao pale wanapopata matatizo,.

Wakili wa kujitegemea, Dk. Aloys Rugazia, amesema hayo jana, katika viwanja vya shule hiyo, wakati wa maandalizi ya kutoa elimu ya sheria bure na kuandaa nyaraka, kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao hawana fedha za kupata huduma hiyo.

"Kwa siku ya Jumatano tumejipanga kutoa mafunzo, kwa baadhi ya wanafunzi wa sekondari kuhusu misingi ya haki na lengo ni kuwatia moyo, wafahamu tasnia ya sheria inahusu nini na inaweza kutumika vipi katika kusaidia jamii, huku elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi. 

"Wanafunzi wana wazazi na wazazi ni sehemu ya Watanzania, elimu watakayoipata itafika mbali na kwa upana, tumewapa fursa kubwa wananchi wa Temeke kunufaika na wiki hii ya sheria," amesema Dk. Rugazia 

Pia, amesema eneo la jinai za kuoneana na kubambikiawa kesi husumbua watu wengi katika jamii, huku wananchi wakilalamika.

Amesema changamoto nyingine ambayo wananchi wanapata ni eneo la ardhi na mirathi wajane, wazee na  watoto yatima wakipata shida kupata haki zao za msingi kwa wakati.

"Ardhi ni maisha ni moja kati ya mali muhimu katika mustakabali wa watu mara nyingi ardhi imekuwa ikileta msuguano kwa walionacho na wasio nacho, mara nyingi wanajikuta katika hali ngumu ndiyo maana kwa wiki hii tunatoa msaada bure watu waje.

Amesema kuwa wapo kwenye Wiki ya Sheria, ambayo ilizinduliwa Januari  25, 2025 kwa kawaida wanaadhimisha kwa kuifikia jamii kuhakikisha inapata haki, kwa sababu sio kila mtu anauwezo wa kulipia gharama za kupata huduma za kisheria.

"Mimi nikiwa kama Managing Partner wa Kampuni ya Sheria ya Afrifa Legal Consultant, kwenye hii wiki, tumeamua kwa udogo wetu kutoa hudumua hii, kwa wana Temeke," amesema,