SERIKALI imefanya maboresho kwa kuongeza viwango vya posho za kujikimu wasimamizi wa uchaguzi kupitia waraka wa utumishi wa umma namba moja uliotolewa Mei 24, 2022.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, ametoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Angelina Malembeka.
Mbunge huyo amehoji Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mpango wa kuongeza posho kwa askari na maofisa wasimamizi wa uchaguzi.
Katambi amejibu kuwa wakati wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa ngazi ya jimbo na kata hulipwa posho za kujikimu wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya uchaguzi kwa kuzingatia waraka huo.
Aidha, amesema kwa upande wa watendaji na walinzi wa vituo vya kupigia kura, utaratibu wa uboreshaji wa viwango vyao vya posho utazingatiwa wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na bajeti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika maswali yake ya nyongeza, Mbunge huyo alisema kwa kuwa uboreshaji wa daftari utakwenda sambamba na uboreshaji posho kwa mwaka 2025, na kuhoji serikali haioni haja ya kuanza kulipa mwaka huu katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuleta motisha kwenye uchaguzi.
“Zanzibar maofisa husimamia chaguzi mbili hawaoni umuhimu wa kulipa posho mbili maana husimamia uchaguzi wa Rais Zanzibar na Wawakilishi na uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge,” amehoji.
Akijibu maswali hayo Katambi amesema waraka huo umeanza kutekelezwa na wanazingatia mapendekezo hayo kwa mujibu wa sheria, miongozo na taratibu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED