Walimu wakutana kutafuta mwarobaini wa miandiko mibaya kwa wanafunzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:37 PM Jun 14 2024
Mkurugenzi wa Shule za Waja Springs, Chacha Wambura akizungumza na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Mji wa Geita waliokutana katika shule hiyo ili kujengeana uwezo wa namna gani ya kuwasaidia wanafunzi wenye miandiko mibaya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Shule za Waja Springs, Chacha Wambura akizungumza na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Mji wa Geita waliokutana katika shule hiyo ili kujengeana uwezo wa namna gani ya kuwasaidia wanafunzi wenye miandiko mibaya.

Mabadiliko ya mfumo wa mitihani ya darasa la saba unaotarajiwa kufanyika Septemba 2024 huenda ukawaathiri wanafunzi wenye miandiko mibaya kama juhudi za maksudi hazitachukuliwa kuwasaidia wanafunzi hao kabla ya muda wa mtihani kufika.

Zaidi ya miaka mitano iliyopita utungwaji wa mitihani kitaifa ulikuwa wa muundo wa kustalisha ambapo mwanafunzi alikua akichora mstari kwenye jibu, lakini kwa mabadiliko yaliyofanywa na Wizara ya elimu mapema mwaka huu, wanafunzi watalazimika kujibu maswali kwa kuandika jibu.

Hayo yamesemwa juzi Juni 12,2024 na walimu wa shule za msingi za Halmashauri ya Mji wa Geita waliokutana kubadilishana uzoefu na walimu wa shule ya msingi binafsi ya Waja Springs ambayo imekuwa ikiwafundisha wanafunzi wake kuandika mwandiko mmoja unaofanana.

Mwenyekiti wa Umoja wa waalimu wakuu wa shule za Msingi Halmashauri ya Mji Geita Ndatu Said, alisema walimu hao wamekutana kuona namna gani wanafunzi wa madarasa ya mitihani wataweza kufanya vizuri kwenye mitihani ijayo ya kitaifa.

“Tulifanya mtihani wa kanda umehusisha mikoa sita lakini hali si nzuri sana hasa kwenye mwandiko hii imekuwa ‘format’ mpya kwao ya namna ya ujibuji mtihani awali ilikua OMR lakini Januari tuliletewa barua kuwa ‘format’ (muundo) imebadilika wanafunzi watalazimika kuandika majibu na tumebaini wanafunzi  wetu sio wazoefu wa miandiko mizuri ndio mana tunatafuta mbinu za kuwasaidia“ alisema Said

Alisema athari ya mwandiko mbaya zinaweza kupelekea mwalimu anaesahihisha kumnyima maksi mwanafunzi kutokana na mwandiko mbaya licha ya kuwa amejibu swali kwa usahihi.

Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalangalala, Regina Kitau alisema mwanafunzi kuwa na mwandiko mbaya kunamfanya aandike kitu kisichoeleweka  na inapotokea  msaihishaji sio mwalimu wake atashindwa kusaihisha na matokeo yake mwanafunzi atafeli mtihani hata kama ameandika majibu sahihi.

Alisema athari za mwandiko mbaya zitaonekana zaidi mwaka huu lakini kwa miaka ijayo hali itakuwa tofauti kutokana na walimu kuamua kubadilishana uzoefu huku madarasa ya chini mkwazo ukiweka kwenye somo la KKK yaani kusoma,kuandika na kuhesabu.

Walimu wakuu kutoka shule za Msingi za Halmashauri ya Mji wa Geita wakiwa kwenye semina ya kuangalia namna gani ya kuwasaidia wanafunzi wa madarasa ya mtihani wenye miandiko mibaya ili waweze kufanya vizuri kwenye mtihani wao wa kuhitimu darasa la saba.
Ofisa elimu taaluma wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Khadija  Ubuguyu akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu zaidi ya 200 wa shule za Msingi alisema wamelazimika kukutana ili kupata utaalamu kutokana na shule hiyo kuwa na wataalamu wa kuumba herufi.

“Tunaenda kwenye mtihani ambao umebadilishwa mfumo wake zamani watoto walikua wakichora mstari kwenye jibu  kupitia OMR sasa mfumo umebadilishwa watoto wanatakiwa waandike majibu kwa mikono yao utafiti tuliofanya tumegundua hali sio nzuri kwa miandiko ya watoto” alisema Ubuguyu.

“Lakini pia tumegundua Waja Springs wana wataalamu wa kuumba herufi hii imewasaidia wanafunzi wao kuwa na mwandiko mmoja unaofanana tukaona kumbe inawezekana kuwa na mwandiko mmoja kwa halmashauri nzima ndio maana tukaomba msaada tuje tujifunze ili kuifanya halamshauri yetu ifanye vizuri”

Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa kampuni za Waja Chacha Wambura, alisema Serikali imefanya kazi kubwa kwenye sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kujenga vyumba vya madarasa,kuajiri walimu na kupandisha madaraja hivyo walimu wakuu nao wanapaswa kujenga dhana ya uwajibikaji ili shule zao ziweze kufanya vizuri.

“Suala la uwajibikaji kwa wakuu wa shule haliepukiki, Mwalimu mkuu wewe ni picha ya shule unapaswa uwe makini unapotaka kufanya jambo  wasimamie walimu hakikisha wanafundisha na wanafunzi wanaelewa” alisema Wambura

Halmashauri ya Mji wa Geita ina shule 97 za Msingi kati ya hizo 68 ni za Serikali na 29 ni binafsi zote zikiwa na wanafunzi zaidi ya 90,000 wa darasa la kwanza hadi la saba.