WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ameridhia kupandishwa hadhi Halmashauri ya Mji wa Kibaha, kuwa Manispaa.
Mchengerwa ameyasema hayo Januari 27, 2025 aliposhiriki hafla ya kuunga mkono maazimio ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea pekee wa urais;Pamoja na mgombea Mwenza Balozi Emmanuel Nchimbi, huku upande wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akiteuliwa kuwa mgombea urais Zanzibar.
Akiwa katika hafla hiyo, ilivyofanyika Mailimoja Mjini Kibaha, Mchengerwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, akitokea Mkoa wa Pwani, amesema rais ameridhia ombi hilo na kwamba michakato mingine itaendelea kukamilisha miradi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Mlao, amesema chama hicho kwa mkoa huo, kinaungana na maazimio ya Mkutano Mkuu, kwa wagombea wakliopitishwa kugombea nafasi hizo.Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Sylvestry Koka, amemshukuru rais, kwa kuridhia kupandisha hadhi halmashauri hiyo kuwa manispaa, baada ya maombi ya muda mrefu.
Amesema hayo yote yametokana na Mmaendeleo yaliyofanyika na kwamba wanaendelea kujenga mji huo, kama ambavyo umekwisha kupangwa , ili uendelee kuwa wa kisasa.
"Leo ni siku ya furaha na tunaipongeza serikali yetu kwa uamuzi walioufikia, baada ya maombi yetu ya muda mrefu kuhakikisha mji wetu wa Kibaha sasa unakuwa Manispaa," amesema
Amesema yaliyofanyika tangu aingie madarakani 2010 ni mengi katika mji wa Kibaha, jambo ambalo linastahili halmashauri hiyo kuwa Manispaa.
"Wakati naingia madarakani eneo la lami lilikuwa ni barabara ya Tamko kupitia Hospitali ya Rufaani ya Mkoa wa Pwani Tumbi, tofauti na sasa kilomita 21 zimepatikana na kila kata ina lami," amesema.
Koka amesema changamoto pekee iliyobaki kwa sasa, ni maji katika kata ya Pangani, ambayo inaendelea kushughulikiwa na hivi karibuni itatatuliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED