Siri upigaji serikalini hii hapa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:08 AM Apr 28 2024
CAG mstaafu, Ludovick Utouh.
PICHA: MAKTABA
CAG mstaafu, Ludovick Utouh.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, amesema kukosekana uadilifu ndicho kiini cha kuendelea kuripotiwa vitendo vya rushwa na ufujaji wa fedha za umma.

Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati Taasisi ya WAJIBU ambayo yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wake, ilipowasilisha uchambuzi wa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23.

Uchambuzi wa taasisi hiyo unaonesha kuwa fedha za serikali ambazo ziko hatarini kupotea kutokana na viashiria vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu ni Sh. bilioni 1,770.84 kwa mwaka 2019/20, Sh. bilioni 4,590.73 mwaka 2020/21, Sh. bilioni 3,084.55 mwaka 2021/22 na Sh. bilioni 2,778.01 mwaka 2022/23.

Amesema dosari hiyo kiutendaji inatokana na watumishi wa umma kukosa uadilifu, hivyo kutumia fedha za umma kwa manufaa yao binafsi.

Ametoa mfano, utata ulioripotiwa na CAG katika ripoti yake ukaguzi wa mwaka 2022/23 ambamo anasema Wizara ya Maliasili na Utalii iliingilia katika mazingira yenye utata zabuni iliyotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Mamlaka hiyo imetangaza zabuni ya ujenzi wa jengo la makao makuu yake ambayo mshindi wake alitangazwa Machi 9, 2022 baada ya mchakato wote wa zabuni kukamilishwa kisheria, zabuni ikiwa na thamani ya Sh. bilioni 9.8.

Hata hivyo, CAG anaripoti kuwa Aprili 21, 2022 zabuni ilisitishwa kwa maelekezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii, iliyoagiza zabuni itangazwe upya, lakini mshindi akawa yuleyule alishinda zabuni ya kwanza, lakini kukawa na ongezeko la Sh. milioni 686.6 kutoka Sh. Bilioni 9.8 za awali hadi bilioni 10.4. Pia kukawa na gharama nyingine ya mchakato wa zabuni Sh. milioni 16.08.

Akifafanua hoja yake, Utouh amesema: "Tatizo si sheria, tatizo ni sisi na ukosefu wa uadilifu.

Hilo ndilo tatizo letu kubwa. Na huu mfano wa NCAA, ninawashukuru TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kusema kwamba mnalichunguza.

"Iko wazi kwamba ile ni mtu aliona zabuni imepita, 'itapitaje mimi sijapata changu? Akaagiza zabuni isitishwe. 'Rudieni', halafu akaweka hapo cha kwake. Liko wazi hili, ni suala la uadilifu".

Utouh amesema wakati mwingine yatakuwa yanafanyika marekebisho ya sheria, lakini hayatakuwa na maana kama watumishi wa umma na jamii haitakuwa na uadilifu.

"Hata huu mfumo mpya wa ununuzi wa umma (NeST), ni mfumo mzuri, lakini tumekuwa na matatizo nchini, watu kukataa kutumia mifumo.

"Sasa swali ni hili, kwa NeST hii, mtakuwa na mbinu gani ya kulazimisha watu ambao wanakataa kutumia mifumo kwa sababu zao binafsi za kujinufaisha?", Utouh alihoji, akielekeza hoja kwa watendaji wakuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) waliokuwamo ukumbini wakati wa wasilisho la uchambuzi huo.

Amesema katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (halmashauri), kuna sheria ya kutumia mashine za POSS, lakini CAG kila anapokagua anakuta fedha zimekusanywa na hazijapelekwa benki.

"Kwahiyo, hoja si mfumo, bali hoja ni uadilifu wetu sisi. Na ninafikiri hili tupigie kelele sasa nani atamfunga paka kengele? Serikali ni watu; mimi, wewe na yule, Mama Samia na kila mtu, ndiyo serikali! Na kinachoporwa na kinachopigwa ni mali ya nani? Ni mali yako wewe na mimi.

"Tufanyaje? Ni vikao kama hivi tuelimishane, kupeana taarifa ili sisi wananchi tupige kelele.

Tukipiga kelele, hiyo serikali ambayo imetulia, itashtuka, itaamka na kuchukua hatua.

“Kwa hiyo, mimi niseme kwamba kubwa ninaloliona mimi, yote haya ya rushwa na 'madudu' mengine serikali ukweli ni tabia zetu, ni ubinafsi wetu, ile tamaa ya kujilimbizia mali, ambayo imekubuhu kwa watumishi wengi wa serikali na hata watumishi wa sekta binafsi.

"Rushwa iko pande mbili. Si tu kwamba rushwa iko kwa watumishi wa serikali, mara nyingi nao wanapigwa na sekta binafsi.

"Rushwa iko kote, serikalini na sekta binafsi, ingawa zinazopigwa nyingi zaidi ni za serikali kwa sababu ni rahisi kuzipiga zile. Ndiko zinapigwa nyingi zaidi," amesema, ukirejewa uchambuzi wa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2021/22, uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU, umebainishwa miamala mbalimbali yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu wa fedha za umma.

Katika uchambuzi wake, taasisi hiyo imebaini kwamba kiasi ambacho aidha hakikukusanywa au kimetumiwa na serikali pasi na kupata tija yoyote (nugatory expenditure) kimepungua kwa asilimia 33 kutoka Sh. bilioni 4,590.73 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh. Bilioni 3,084.55 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Vilevile, uchambuzi umebaini kuwa mashirika ya umma yamekuwa na ongezeko la asilimia 43 ya jumla ya miamala ambayo ina viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kutoka Sh.

bilioni 1,408.36 mwaka wa fedha 2020/21, hadi Sh. bilioni 2,015.78 mwaka wa fedha 2021/22.

Hii ina maana kwamba jumla ya miamala yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu katika mashirika ya umma pekee ni Sh. bilioni 2,015.78 sawa na asilimia 65 ya jumla ya miamala yote yenye viashiria vya rushwa ubadhirifu na udanganyifu ya Sh. Bilioni 3,084.55 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Kwa ujumla, katika uchambuzi wake huo, Taasisi ya WAJIBU imebainisha miamala mbalimbali yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu wa fedha za umma, ikisababisha hatari ya upotevu wa Sh. bilioni 1,770.84/- mwaka 2019/20, Sh. Bilioni 4,590.73 mwaka 2020/21 na Sh. bilioni 3,084.55 mwaka 2021/22.

Hii ina maana kwamba, jumla ya Sh. trilioni 9.446 ziko hatarini kupotea katika mazingira yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu katika miaka mitatu ya fedha (2019/20-2021/22).

Kiasi hicho kama kingelielekezwa kutatua uhaba wa miundombinu shuleni, kingelitosha kujenga vyumba vya madarasa mpya 472,306 au matundu milioni 8.587 ya vyoo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chumba kimoja cha darasa kinajengwa kwa Sh. milioni 20 kikiwa na samani zake zote huku tundu moja la choo likijengwa kwa Sh. milioni 1.1. Sh. trilioni 9.446 zilizo hatarini kupotea, kama zingeelekezwa kwenye sekta ya afya, zingetosha kujenga hospitali 1,246 za wilaya au vituo vya afya 8,056 au zahanati 31,419.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, ujenzi wa zahanati unagharimu wastani wa Sh. 300,641,028 (vifaa vinagharimu Sh. 87,677,593.70); ujenzi wa kituo cha afya unagharimu wastani wa Sh. 1,172,583477 kikiwa na majengo 11 (vifaa vinagharimu Sh. 501,728550) huku ujenzi wa hospitali ya wilaya ukigharimu Sh. bilioni 5.781 (vifaa vinagharimu Sh. bilioni 3.4).

Kimsingi, kuwapo hatari ya upotevu wa fedha za umma iliyoibuliwa na CAG ilhali nchi inakabiliwa na uhaba wa miundombuni na samani shuleni, kunakwaza utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).

Mpango huo umebainisha malengo muhimu katika sekta ya elimu yanayotakiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2026, ambayo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa madawati na vitabu, kuboresha uwiano wa vyoo na mazingira ya kazi kwa walimu katika ngazi zote, malipo yao na makazi kuwa karibu na maeneo ya kazi.

Hatari hiyo ya upotevu wa mabilioni ya shilingi ilhali nchi bado inakabiliwa na uhaba wa vituo vya kutolea huduma za afya, unakwaza utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa mwaka 2008 unaoelekeza serikali kuhakikisha kunakuwa na zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata na hospitali kwa kila wilaya nchini.