SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu mkopo nafuu wa Dola za Marekani bilioni 2.5 (sawa Sh. trilioni 6.7) uliotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini na kuzua maswali baada ya habari yenye dosari kama ilivyotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa.
Ufafanuzi huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mohbare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upotoshaji uliofanywa na vyombo hivyo.
“Korea haijapewa sehemu ya bahari yetu tunachofanya ni kushirikiana nao kupata uzoefu na utaalamu kutoka kwa rafiki zetu hao ili kuboresha shughuli zetu za uvuvi kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu na teknolojia mbalimbali,” alisema.
Alisema sio Tanzania pekee inayopata mkopo wa aina hiyo na kufafanua kuwa ziko nchi 59 ambazo zimekwishapata mikopo ya aina hiyo kwenye mabara ya Afrika, Asia na Ulaya na haziweki rehani mali zake.
Alisema taarifa hizo zilisambaa jana kwenye mitandao ya kijamii na kwenye mashirika ya habari ya kimataifa yakiwamo baadhi ya magazeti ya Afrika Mashariki na kusababisha taharuki kubwa.
Alisema kwenye ziara hiyo Rais Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia utiaji saini wa nyaraka tatu ambazo ni mkataba na nyaraka zingine mbili ni za makubaliano (MoU) na tamko la pamoja baina ya mataifa hayo mawili.
Alisema katika mkataba ambao Rais Samia ameshuhudia utiaji saini wake unahusu mkopo wa Dola za Marekani bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu chini ya mfuko wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Korea (IDCF).
“Mkopo huu kama ulivyoelezwa na Balozi wetu Korea, Togolani Mavura na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, huu ni mkopo wa masharti nafuu na utatolewa ndani ya miaka mitano kuanzia sasa na utaanza kulipwa baada ya miaka 25 kupita kwa hiyo tumepewa unafuu huo,” alisema.
“Mkopo huo utalipwa kwa kipindi cha miaka 40 na tunaposema ni mkopo nafuu ni kwa sababu riba ya mkopo huu ni asilimia 0.01 kwa hiyo riba hiyo ni ndogo sana. Serikali haijaweka rehani kitu chochote wala mali yoyote kama ambavyo imepotoshwa kwenye majukwaa mbalimbali,” alisema.
Kadhalika, mkopo huo hauna masharti ya kuweka rehani kitu chochote na sio mara ya kwanza kwa Tanzania kupata mkopo wa aina hiyo chini ya mfuko huo IDCF.
Alisema Tanzania imeshapata mkopo wa aina hiyo mara mbili na mara ya kwanza ilipata Dola za Marekani milioni 733 mwaka 2014-2022 na mara ya pili ilipewa mkopo wa Dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka 2021-2025.
Baadhi ya miradi mingine iliyotokana na ushirikiano baina ya Tanzania na Korea na mikopo ya aina hiyo iliyotajwa ni ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila, uboreshaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam, Daraja la Jakaya Kikwete, Mto Malagalasi na uunganishaji wa Mkoa wa Kigoma kwenye gridi ya taifa ya umeme.
Mingine ni mradi wa majisafi na taka mkoani Iringa, awamu ya kwanza ya mradi wa vitambulisho vya taifa vya NIDA, Bandari ya Uvuvi Bagamoyo, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar.
Kadhalika, mradi wa Hospitali ya Binguni Zanzibar, Chuo cha TEHAMA jijini Dodoma na mradi wa umwagiliaji Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED