Rekodi yako ikichafuka kwenye ukopaji unafungiwa miaka sita

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 01:56 PM Feb 26 2025
Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Deogratius Mnyamani.
PICHA:SALOME KITOMARI
Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Deogratius Mnyamani.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuwa kwa mtu yeyote anayekopa na kutorejesha kisha kutambuliwa na kanzidata kama mkopoji sugu mwenye mkopo chechefu atafungiwa kupata huduma hizo kwa miaka sita hadi kusafishwa.

Akiwasilisha mada ya mafanikio na changamoto za usismamizi wa sekta ya huduma ndogo za fedha, Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Deogratius Mnyamani , amewaambia waandishi wa Habari Februari 26,2025 mjini Mtwara, kwamba licha ya BoT kusimamia madaraja manne ya huduma ndogo za fedha kasi kubw ainaonekana kwenye Daraja la pili ambalo ni la watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana.

Amesema kila mmoja ana historia ya ulipaji wa mikopo lengo ni kujia tabia ya urejeshaji wa mikopo na kwmaba mitandao yote ya simu imeingia kwenye mfumo huo.

“Rekodi yako ikishachafuka kuisafisha ni miaka sita mbele, achana na uliyochafuka kwa makosa ya bahati mbaya kwamba ulishalipa ila mtoa huduma akuiweka vizuri, na kama si mlipaji mfumo unakwenda kadi kwenye kodi ya ardhi na ankra za maji,utaonekana hujalipa,”amesema.

Mnyamani amesema mfumo huo umewekwa ili ksuaidia taasisi za fedha zijue zinayemkopesha ana historia gani na kama fedha anzoomba anaweza kuzilipa.

“Ukiona imefika Januari na unatakiwa kulipa deni, ustaarabu unasema usizime simu au kuhama mtaa, bali muarifu mtoa huduma ajue sababu za kutetereka, sio umwambie nilienda Dubai Desemba lakini ukisema biashara zimeteteraka kwasababu ya ukame, magonjwa ya mlipuko. Mnakubaliana namna ya kuliweka vizuri deni husika.

“Watanzania wengi wakishaona hawawezi kulipa wanakimbilia kuzima simu na kuhama, mwisho wa siku unamtia kichaa mtoa huduma anaona mtaji wake unaenda kuzama,”amesema Mnyamani.

“Tunaona sasa haya yanatumiwa na taasisi ndogo za fedha, kwasasa hazikjoeshi kienyeji na lengo letu ni kuondoa mikopo chechjefu iwe chini ya asilimia 5, nchi nyingine wamekuja kujifunza kwenye hili,”amesema.