Miradi, taasisi 180 yachunguzwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 06:04 AM Apr 20 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

SERIKALI imesema imeanza uchunguzi wa miradi ya maendeleo 179 yenye thamani ya Sh. bilioni 61.01 iliyobainika kuwa na kasoro mbalimbali katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo 1,086 yenye thamani ya Sh. bilioni 743.9 iliyofanyika kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, akizungumza bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25, alisema hayo na kuomba kuidhinishiwa Sh. trilioni 1.10.

Kadhalika alisema, uchambuzi wa mifumo 446 umefanyika kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika maeneo ya huduma za jamii, fedha, majengo, utawala, usafirishaji, biashara, umeme, kilimo na misitu.

Alisema upungufu huo unaochunguzwa ulibuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), katika mwendelezo wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2024/25 kupitia Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), wanatarajia kufanya ukaguzi wa kawaida katika Taasisi za Umma 180 na Ukaguzi Maalum katika Taasisi za Umma 10 kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.

UPATIKANAJI WATAALAMU UTUMISHI

Simbachawene alisema katika mwaka 2024/25 ofisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuwezesha kupatikana wataalam katika Utumishi wa Umma maeneo ya vipaumbele ambayo ni pamoja na usimamizi michakato ya ajira ili kuwezesha waajiri kupata watumishi wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa miundo ya utumishi husika.

Vilevile, watumishi kupatiwa vitendea kazi, kuboresha maslahi na mafunzo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi, kutoa taarifa na elimu kwa umma ili kukuza uelewa wa shughuli zinazotekelezwa na sekretarieti hiyo.

Wataimarisha utendaji kazi wa Taasisi kwa kutumia TEHAMA, kuimarisha upatikanaji wa takwimu za ajira; na kuimarisha uwajibikaji na udhibiti wa matumizi ya fedha na shughuli nyingine za sekretarieti ya ajira kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

UTEKELEZAJI PSC

Simbachawene alisema katika mwaka 2024/25 Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) inatarajia kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwamo kufanya ukaguzi wa kawaida katika taasisi za umma 180 na ukaguzi maalum katika taasisi za umma 10 kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.

Pia, atafanya mikutano minne kujadili na kutolea uamuzi rufaa, malalamiko, taarifa za masuala ya kiutumishi na kuhuisha miongozo ya Tume ya Uzingatiaji wa masuala ya Kiutumishi; kuelimisha wadau 1,500 katika Taasisi za Umma na Serikali za Mitaa kuhusu majukumuya Tume na uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma na kuwajengea uwezo watumiaji 1,300 wa Mfumo mpya wa kielektroniki wa kushughulikia rufani.