MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Watanzania wanachopaswa kutambua na kukiweka akilini kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani ni kwamba, mpambano utakuwa ni wao na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amewataka askari wa Jeshi la Polisi, kuacha mpambano huo uchezwe kama mechi ya Simba na Yanga kwa kusimamia kiapo chao cha kulinda raia na mali zao, kwa kuwa mali za raia nyingine ni pamoja na kura zao.
Mbowe ameitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Waso, Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro jijini Arusha.
“CCM hakitaki hoja ya Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, hawataki kwa sababu wanajua wakienda kwenye uchaguzi ulio huru na wa haki, watawatandika asubuhi misa ya kwanza.
“Tumewaambia wenzetu tunataka Tume Huru ya Uchaguzi, tunataka Katiba Mpya ili uchaguzi wetu uwe huru na haki, hawataki.
“Nimeona askari polisi hapa, niwaambie ndugu zangu wa polisi, mateso wanayoyapata Watanzania wote ni pamoja na ninyi. Na mateso haya yanasababishwa na CCM. Acheni kuwa machawa wa CCM, acheni kuwasaidia CCM. Simamieni haki katika nchi yetu,” amesema.
Amewaeleza askari polisi kwamba, wamekula kiapo cha kulinda raia na mali zao, hivyo mali za raia ni pamoja na kura zao.
“Askari wetu simamieni kiapo chenu, msiwe mawakala wa kuisaidia CCM. Tuachieni hiyo ngoma tucheze nao kama Simba na Yanga,” amesema Mbowe.
Amesema wananchi wa maeneo ya Loliondo, wamewaambia hawako tayari kuirejesha CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mkutano uliofanyika Jumamosi, Mang'ola na Eyasi, Wilaya ya Karatu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu, amehadharisha kwamba, Maofisa Watendaji wa Vijiji (VEO), watakaoengua wagombea wao katika mchakato huo, hawatabaki salama.
“Mimi ninasema mchana kweupe. Ofisa mtendaji wa kijiji atakayeengua mgombea wetu yeyote; hawa watendaji wanakaa wapi, si wanakaa na sisi mitaani huku, akiengua mgombea wetu mwambieni kabla hatujafika huko, ukiengua mgombea wetu hubaki.
“Achilia mbali kuwa Mwenyekiti wa Kijiji au Kitongoji, ninataka tushindwe kwenye kura tu. Tunataka wananchi watukatae kwenye kura tu, tusishindiwe mezani, tusishindwe kwa wagombea wetu kuenguliwa,” amesema Lissu.
Amesema kwa sasa wana jukumu la kujipanga kwa mwaka ujao kurudisha heshima ya Karatu na Mang'ola, warudishe uchumi wake na rasilimali zake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED