MAUAJI MWENYE UALBINO: Paroko, mganga, baba wakamatwa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:57 AM Jun 20 2024
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime.
Picha:Maktaba
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime.

WATU tisa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kukutwa na viungo vinavyodhaniwa vya mwenye ualbino mkoani Kagera wakiwa wamevihifadhi katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja.

Kati yao, wamo Paroko Msaidizi wa Bugandika, Elipidius Rwegoshora, mganga wa jadi, Desideli Evalist, mkazi wa Nyakahama na Novart Venant, ambaye ni baba mzazi wa mtoto Asimwe Novath (2), aliyechukuliwa mikononi mwa mama yake Mei 30 mwaka huu na watu wasiojulikana na mwili wake kugundulika baada ya siku 19, akiwa ameuawa. 

Mwili wa mtoto huyo ambao ulikutwa baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa huku ukiwa kwenye mfuko wa sandarusi, uliopolewa Jumatatu katika karavati linalopitisha maji katika barabara iliyoko Luhanga kwenda Kijiji cha Makongora, mkoani Kagera. 

Katika taarifa Jeshi la Polisi iliyotolewa jana na msemaji wa jeshi hilo nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, ilibainisha kuwa baada ya tukio hilo, jeshi kwa kushirikiana na raia wema, lilifanya msako mkali kuanzia Mei 31 mwaka huu hadi usiku wa kuamkia jana na kukamata watuhumiwa tisa. 

Misime alisema katika taarifa yake hiyo kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya mtoto Asimwe, wakiwa wamevihifadhi katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja. 

"Watuhumiwa waliokamatwa ambao walieleza jinsi walivyoshiriki katika tukio ni baba mzazi wa mtoto, mganga wa jadi na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Rugandika, Rwegoshora, ambaye anadaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu. 

"Pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kumlipia gharama zote za uganga. Watuhumiwa wengine ni Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara na Faswiru Athuman, mkazi wa Nyakahama (wote wilayani Muleba). 

"Wengine ni Gozibert Alikadi, mkazi Nyakahama Kamachumu, Rwenyagira Burkadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Ramadhani Selestine, mkazi wa Kamachumu na Nurduni Hamada, mkazi wa Kamachumu," alisema. 

Misime alisema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu wanaoendekeza imani za kishirikina ikiwamo kupiga ramli chonganishi wakiaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa njia za kishirikina kuacha tabia hiyo. 

"Waache kudanganya kwamba kuna utajiri unaopatikana kwa kumiliki viungo vya binadamu mwenye ualbino, kwani si kweli kwa kuwa kama ingekuwa hivyo, familia zenye watoto au ndugu wenye ualbino wangekuwa na utajiri mkubwa, badala yake tunaona wakiishi maisha ya kawaida kama sisi wengine," alisema. 

Misime aliongeza kuwa wanaofanya vitendo hivyo wanapaswa kutambua ni uhalifu uliopitiliza katika karne hii ya maendeleo ya sayansi na teknolojia kutenda ukatili huo, kwa kuwa yeyote anayefanya na anayeshiriki katika uhalifu wa aina hiyo, lazima atakamatwa kwa kuwa vitendo hivyo havina baraka za Mwenyezi Mungu wala sheria za nchi. 

"Ni vitendo vya aibu kwa anayefanya na kwa familia yake pia, wanalifedhehesha taifa. Watu wenye mawazo hayo waachane nayo, wafanye kazi halali, watoke jasho na ndiyo siri ya kufanikiwa katika maisha na si kuendeleza ushirikina na kupiga ramli chonganishi," alisema. 

Juzi Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa kifo cha mtoto mwenye ualbino kimemgusa, huku akitaka washiriki wa Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari, alilokuwa analifungua, kusimama kwa muda na kuomba kwa ajili ya kundi hilo.