GGML yawajengea Polisi nyumba za Shilingi bilion 1.8 Geita

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:43 PM Oct 06 2024
GGML yawajengea Polisi nyumba za Shilingi bilion 1.8 Geita
Picha:Mpigapicha Wetu
GGML yawajengea Polisi nyumba za Shilingi bilion 1.8 Geita

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML) imetumia zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba sita za maofisa wa polisi Mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya Uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR). Kujengwa kwa nyumba hizo kumelenga kutoa makazi ya kisasa kwa maofisa wa polisi na kuimarisha utendaji kazi wa jeshi hilo pamoja na kuwafanya wafanye kazi kwa ufanisi na kuchangia ulinzi na usalama kwa wananchi.

Nyumba hizo zimezinduliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa  Wizara ya Mambo ya ndani na viongozi wa mkoa wa Geita. 

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyumba hizo Makamu wa Rais wa Anglogold Ashant anaeshughulika na masuala ya uendelevu na Mahusiano Afrika, Simon Shayo amesema  bila usalama hakuna mtu wala biashara inayoweza kufanikiwa.

Amesema uamuzi wa kusaidia vyombo vya dola umelenga kuchangia katika jamii yenye amani na ustawi na kwamba ubia baina ya polisi na mgodi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu kwa watu waliokuwa wakiingia mgodini bila kibali.

Aidha kupitia ubia huo, wameanzisha polisi jamii na kufanya kuwa  ubia wa mfano.  “Tulichokifanya hapa tumeanza kujaribu kukifanya kwa nchi nyingine tunazofanya kazi tunahangaika na matukio ya uhalifu na unavyofahamu huwezi kuwa na mgodi salama kama jamii inayokuzunguka sio salama”amesema Shayo

 “Usalama wetu na wa watu wanaoishi karibu na shughuli zetu ni muhimu sana, na tunajivunia kuwa washirika katika kuhakikisha ustawi wao majukumu yetu kama kampuni inayo wajibika tunaenda mbali zaidi ya uchimbaji madini  yanahusisha ushiriki wa moja kwa moja katika ukuaji wa jamii na umma kwa ujumla” amesema Shayo.

Amesema mgodi huo umejikita katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania, na kuona  hatua kama hiyo ni njia ya kusaidia juhudi za Serikali katika kujenga jamii zenye nguvu, salama na zilizo na ulinzi.

“Tunafahamu usalama ni nguzo ya maendeleo, bila usalama hakuna mtu wala biashara inayoweza kufanikiwa kwa kusaidia vyombo vya dola, tunalenga kuchangia katika jamii yenye amani na ustawi"amesema Shayo
Aidha mbali na kuimarisha makazi ya maofisa wa polisi ipo miradi mingine ikiwemo ujenzi wa ofisi pamoja na nyumba ya kuishi kamanda wa polisi Mkoa,ujenzi wa vituo vya polisi jamii,ununuzi wa pikipiki 50 za askari kata pamoja na kufadhili mafunzo kwa vijana wanaoimarisha ulinzi kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi kazi ambayo imesaidia kupunguza uhalifu kwenye Mkoa huo.

Kwa upande wake Kamada wa polisi Mkoa wa Geita Saphia Jongo amesema makabidhiano ya nyumba hizo ni uthibitisho wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji. 

Amesema kujengwa kwa nyumba hizo ni makubaliano kati ya jeshi la Polisi na GGML na kwamba mradi huo utachangia kuimarisha utendaji wa maofisa na kuwafanya wafanye kazi kwa ufanisi na kuchangia ulinzi na usama kwa watu.

Naibu Waziri wa mambo ya ndani Daniel Siro akizungumza kwenye uzinduzi huo , ameitaka jamii hususan migodi kushirikiana na jeshi la polisi katika miradi ya kimkakati ya kuimarisha mifumo ya usalama ya raia na mali zao na kutunz autulivu wa nchi.