MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesimulia namna alivyookolewa na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo katika sakata la makontena ya vifaa vya ofisi za walimu wa Dar es Salaam kwa kuwa kuna watu walitaka kumchomekea matrekta na magari kwenye makontena hayo.
Makonda aliyasema hayo jana jijini hapa alipokutana na wadau wa mashirika na asasi za kiraia kujadiliana masuala mbalimbali, ikiwemo changamoto zinazowakabili.
Alisema pona yake ni Jenerali Mabeyo kuzuia makontena yasifunguliwe na ulinzi kuendelea kuimarika, la sivyo matrekta na magari yangewekwa katika makontena hayo ili ionekane hakuleta thamani bali ni magari yake.
“Kipindi kile namshukuru Mungu baada ya kugundua taarifa walizozipeleka kwa Rais John Magufuli ni tofauti na uhalisia usiku walitaka kwenda kufungua yale makontena waweke matrekta na magari ili nionekane nilikuwa nadanganya naleta vifaa vya walimu kumbe naleta vya kwangu,” alisema.
Makonda, alisema kulikuwa na wanajeshi wanalinda makinikia ambao wapo chini ya Jenerali Mabeyo walivyowakuta wakaogopa.
“Mabeyo akaweka ngumu hakuna kufunguliwa makontena. Hiyo ilikuwa salama yangu hizi nia njema zina nyakati ngumu sana ... halafu huku nimeshatangazwa huyo mkwepa kodi, fisadi anataka kujitafutia mali,”alisema Makonda na kuongeza kuwa:
“Mimi ni mmoja wa wahanga wa haya mambo ya ufadhili Dar es Salaam nilifanya ile kazi ya ujenzi wa ofisi za nyumba za walimu kwa nguvu kubwa nikaomba wadau wa malori, watu wa vituo vya mafuta wakatoa mafuta, Magereza wakatoa watu, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakatoa vifaa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakatupatia askari tukaanza kujenga ofisi za walimu.”
Alisema wakapatikana watu wengine wema kutoka nchini Marekani walijitolea kontena 20 zilizokuwa na thamani.
“Zikaingia siasa pale zilikuwa siasa kali kweli kweli, kumbe kuna jamaa wanasema huyu akiendelea hivi na walimu wakimpenda atatusumbua mbele ya safari,”alisema Makonda.
Alisema wakati anapambana kuleta maendeleo kwa walimu wakae katika ofisi nzuri na kuheshimika kumbe kuna baadhi wanawaza tofauti.
“Nilipigwa fitina ambayo sijawahi kuiona duniani ikafika mahali nikasema sasa watajua Mungu yupo ama hayupo. Nikasema hata wakitafuta wateja hawatauza na atakayenunua atalaaniwa yeye na kizazi chake,” alisema.
Makonda, alisema anakumbuka wakati ule bosi wake alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo, aliandika barua na kuelezea msaada huo, ilishindikana na kuendelea kushikiliwa kooni.
“Njemba zimekaa vikao vya usiku wakati huo sikuwa najua yale maombi ya kusambaratisha vikao vya sirini kwa sasa nimeshayajua sasa ninawakung’uta na vikao vyao vya usiku wanavyovifanya,” alisema.
Alisema anaelewa asasi za kiraia zinapata changamoto sio kwa sababu wanaleta vitu kwa ajili ya kuuza bali wengine ni kuoneana wivu.
Alisema kulikuwa na upungufu wa vifaa kwa ofisi za walimu zaidi ya 400 wanakaa chini ya miti, aliomba wadau, hajatumia fedha ya serikali, mtu mmoja anaungana na mwenzake kuharibu.
“Umoja wa waovu huwa haudumu, wanasambaratika tukikutana wananiambia mheshimiwa vipi nawambia kwa neema nimerudi wewe je? Utasika kwa kweli unatutia moyo sana, tukikutazama,” alisema Makonda.
Alisema kuna mmoja alikutana naye kwenye kahawa akamueleza wao ni wale wa Magufuli wanaonewa. “Nikamuambia acha uongo haukuwa wa Magufuli acha unafiki wewe yaani mtu anataka kutengeneza chuki kama una sifa zako utafanya kazi kama hauna sifa hautafanya kazi,” alisema.
Makonda amezitaka asasi za kiraia zisiwe sehemu ya uchonganishi na kiongozi wa nchi kwani wataharibu taswira ya nchi.
Alisema ni vizuri asasi hizo kuepukana na siasa katika kazi zao kwa kuwa hazina maslahi wala matokeo chanya.
Kwa upande mwingine, Makonda ametangaza harusi yoyote itakayofungwa Arusha kuwa serikali ya mkoa italipia gharama za ukumbi.
“Lakini wafungaji wa hiyo harusi wawe wanatoka nje ya mkoa wa Arusha, lengo letu kwenye low season na high season tuwe na shughuli kila wakati yaani mkoa wetu uwe unaendelea, tunataka hela iendelee kumiminika katika mkoa wetu,” alisisitiza.
Alisema mwezi ujao kuna 'Masai Festival', tayari wazungu 2,000 wamekubali kushiriki.
“Pia tuna Land Rover Festival mpaka sasa watu waliojitokeza ni wengi. Tumechukua Land Rover kwa kuwa zipo za aina mbalimbali, tumeita watu nchi nzima, tutakuwa na siku tatu kuanzia Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu,” alisema.
Alisema tayari Land Rover 700 zimejisajili hadi sasa, watakutana katika maeneo ya utalii jijini Arusha kufurahia utalii uliopo.
“Kiukweli mtatusamehe huko barabarani mpaka sasa gari zilizojiorodhesha ni Land Rover 700 tunachokifanya tunatafuta maeneo yenye utalii tunapaki magari yetu na kwenye hayo magari kutakuwa na mahema tunakula maisha,” alisema Makonda.
Alisema Mkoa wa Arusha pia, unaandaa mpango maalum wa kupata idadi ya watu wenye ulemavu ili wapatiwe vifaa ikiwemo viti mwendo, miwani na fimbo kwa wasioona.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED