MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameagiza ifikapo Julai 1 mwaka huu, polisi waache kusimamisha magari ya watalii yanayoingia katika jiji la Arusha kwa kuwa tayari wameshakaguliwa katika mipaka na viwanja vya ndege.
Makonda ametoa agizo hilo leo akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Karibu Kili Fair (KKF) yanayofanyika katika viwanja vya Magereza Kisongo jijini Arusha yakijumuisha kampuni zaidi ya 700 za kimataifa kutoka kwenye nchi zaidi ya 50.
"Tumekubaliana kuanzia Julai 1 mwaka huu hakuna polisi kusimakaisha gari za watalii zilizobeba watalii kutoka Airport ama Namanga kuingia katikati ya jiji la Arusha," amesema Makonda
Amesema wanafanya hivyo kwa sababu watalii hao wanakuwa tayari wameshakaguliwa kwenye viwanja vya ndege ama mipakani hakuna sababu ya kuwekewa vikwanzo wengine wanawahi ndege ama ratiba zao.
"Hawa watalii wamekuja kutupatia fedha kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukarimu aliouonyesha kwao lazima watu wa mkoa wa Arusha waonyeshwe kwa ukarimu," amesema Makonda.
Amesema vyombo vyote vinavyohusika na ukaguzi wa wageni wafanye kwenye vituo vya mipaka ikiwemo viwanja vya ndege.
Aidha, Makonda ametoa miezi miwili kwa taksi zinazotumika kubeba wageni na watalii wa Mkoa wa Arusha kuwa na rangi maalumu za kufanana ili kutoa urahisi kwa mtalii kuyafahamu na kulinda usalama wa wageni na watalii.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED