Bunge laanza vikao, muswada kuongeza likizo kwa wanaojifungua njiti kujadiliwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:51 AM Jan 28 2025
Mkutano wa 18 wa Bunge.
Picha: Mtandao
Mkutano wa 18 wa Bunge.

MKUTANO wa 18 wa Bunge unaanza leo vikao vyake jijini Dodoma, huku wabunge wakitarajia kujadili miswada mitano, ukiwamo wa marekebisho ya sheria za kazi.

Miongoni mwa mapendekezo katika muswada huo ni kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa aliyejifungua mtoto njiti kwa kujumuisha na muda uliobaki kufikia 36 za ujauzito.

Vilevile, muswada huo unapendekeza mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30 kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.

Pamoja na hayo, muswada unapendekeza aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi na kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine za misimu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma cha Ofisi ya Bunge, mkutano huo unaanza leo Januari 28 hadi Februari 14 mwaka huu.

Miswada mingine itakayojadiliwa ni ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba Tatu na Nne, Muswada wa Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania na Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Mwaka 2024 na tayari ilishasomwa kwa mara ya kwanza kwenye mikutano iliyopita.

Mkutano huo pia utakuwa mahususi kwa kamati za Bunge kuwasilisha taarifa zake za mwaka kuanzia Januari 2024 hadi Januari 2025 na wastani wa maswali ya kawaida 250 yanatarajiwa kuulizwa na wabunge na kutakuwa na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.