NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amewafunda wanachama wa CCM mkoa wa Shinyanga, kuwa wamoja katika kipindi hiki na kuachana na makundi yasiyokuwa na tija ili kutowapatia mwanya vyama vya upinzani kushinda nafasi mbalimbali za uongozi uchaguzi mkuu ujao.
"Mimi ninapacha wangu niliyezaliwa nae siku, tarehe na mwaka mmoja alinyonya na kuniachia ziwa nami nikanyonya lakini kuna muda tunakosana na tunaelewa hivyo nanyi kama kunamtu kakukosea inabidi msameheane na kukijenga chama kwasababu tunategemeana"Amesema Dk.Biteko.
Dk.Biteko amebainisha hayo leo katika mkutano Mkuu maalum wa jimbo la Msalala Wikayani Kahama ulioandaliwa na Mbunge wa jimbo Iddi Kasimu na kusema, mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi hauhitajiki na badala yake waungane kwa pamoja hata kama hawapendani.
Amesema,wananchi wanataka kuona maendeleo hasa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara na hawataki porojo na migogoro inayoibuliwa ndani ya chama, wakiyakosa yote hayo wanakiadhibu chama sio mbunge wala diwani hivyo makundi yavunjwe.
Amesema, kutofautiana kwenye siasa ni kawaida ila mgorogro usiwe wa kudumu kwani kila mmoja anamtegemea mwenzake,wananchi wakikosa maendeleo watakiadhibu chama na kumpatia mpinzani na lengo ni kuangalia maendeleo ambayo wameyakosa hivyo kila mmoja anawajibu wa kuvunja makundi ili kuwa na lugha moja hasa wanapoelekea kwenye ujaguzi mkuu ujao mwaka huu.
Mbunge wa jimbo la Msalala Iddi Kasimu alitumia kikao hicho katika kuwaomba radhi watumishi wa halmashauri ya Msalala kama kunasehemu walipokoseana kwani yote aliyafanya ni katika kuwasukuna kutekeleza ilani ya uchaguzi na kuhakikisha wananchi wanapata.
Mwanachama wa CCM wa kata ya Bulyanhulu Suzan Swai amesema, chama kinatakiwa kuwachukulia hatua wanachama wake wanaunda makundi na kuandaa wagombea, kuwapitisha kwa wananchi na kuwasumbua viongozi walipo kwani wanasababisha wawe na hofu ya uchaguzi na kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita amesema,serikali imeendelea kuboresha sekta mbalimbali ili kuwasogezea huduma wananchi karibu na sasa hakuna mjamzito anayeweza kujifungulia njiani au nyumbani kwa sababu kila kijiji kuna zahanati, kata kituo cha afya na wilaya hospitali za wilaya ukilinganisha na hapo awali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED