Aliyefungwa maisha kwa kubaka aachiwa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:51 AM Jun 08 2024
Jengo Mahakama ya Rufani Tanzania.
Picha: Maktaba
Jengo Mahakama ya Rufani Tanzania.

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imemwondolea adhabu ya kifungo miaka 30 jela, kifungo cha maisha na fimbo 12 Zilam Hamisi, aliyehukumiwa kwa kubaka na kuwalawiti wanafunzi wawili.

Hatua hiyo imetokana na mahakama kubaini upungufu katika ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Mahakama hiyo mbele ya jopo la majaji Barke Sehel, Panterine Kente na Gerson Mdemu, ilitoa hukumu hiyo jana baada ya kupitia hoja za kupinga adhabu zilizowasilishwa na mrufani.

Wakati ukisomwa uamuzi huo, Mahakama ilisoma ushahidi uliotolewa katika shauri lililodaiwa Oktoba 5, 2018 kwamba baada ya saa za shule, wasichana wawili wa shule ya msingi wenye umri wa miaka 11 na 12 walikuwa wamesimama kwenye kituo cha mabasi cha Mzambarauni, wakisubiri basi linalokwenda nyumbani kwao, Gongo la Mboto. 

Inadaiwa kwenye kituo hicho, kulikuwa na mtu aliyesimama nyuma ya wanafunzi hao huku akizungumza kwenye simu yake ya mkononi na kisha akawauliza wasichana wanasoma shule gani.

Wanafunzi hao walimjibu kwamba walikuwa wanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mzambarauni kisha wakasikia mwanamume akimwambia mtu huyo kwa simu kwamba amewapata wasichana hao wawili.

Mwanamume huyo inadaiwa alikata simu na kuwaambia kuwa alielekezwa na mwalimu mkuu wao kuwachukua hadi maktaba ya Chanika Mbande na Mbagala kukusanya vitabu vya shule.

Mtu huyo  inadaiwa akaendelea kuongea na simu akijifanya anazungumza na mwalimu wao mkuu, walimsikia akizungumza kuwaombea ruhusa kwa wazazi wao. 

Inadaiwa kuwa baada ya kukata simu, aliwahakikishia wasichana wasiwe na wasiwasi kwani wazazi wao tayari wamempa ruhusa ya kwenda nao maktaba. 

Wanafunzi hao wanadaiwa walimwamini, wote watatu walipanda basi la kwenda Chanika Mwisho. Baada ya kufika huko, yule mtu akawaambia wamfuate, walilazimika kumfuata, walitembea kwa muda mrefu kwa miguu hadi msituni.  

Inadaiwa wakiwa msituni, mtu huyo alidanganya wasichana kwamba msitu ulikuwa unalindwa na askari, hivyo, wanapaswa kumruhusu kufunga mikono yao kwa kamba ili askari wakitokea angejifanya amewakamata. 

Watoto waliamini na kumwacha afunge, alitaka kufunga miguu yao lakini walipinga ndipo alipotishia kuwaua iwapo wasingemruhusu kufunga miguu yao.  

Inadaiwa aliwafunga miguu, akawavua nguo na alianza kuwabaka na kuwalawiti, mmoja baada ya mwingine baada ya kutimiza lengo lake akawarudisha wasichana Chanika na kuwaacha wakiwa hoi. 

Wazazi wao walipata wasiwasi walianza kutafuta lakini usiku wa manane, wasichana walipata njia ya kurudi nyumbani wakiwa na hali mbaya kwani walikuwa wamepakwa kinyesi juu ya nguo.  

Inadaiwa walisimulia yote kwa wazazi wao, wazazi walipeleka suala hilo katika Kituo cha Polisi cha Gongo la Mboto kisha waathiriwa walipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa uchunguzi wa kimatibabu. 

Daktari wa Amana,  Magreth Ibobo, ambaye aliwafanyia uchunguzi, alibaini wanafunzi walifanyiwa ukatili huo kwa kuwa sehemu zao za siri zilikuwa wazi. 

Askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Stakishari waliweka mtego ili kunasa mkosaji ambapo mrufani alikamatwa Oktoba 10 mwaka 2018 katika Kituo cha basi cha Mzambarauni akiwa na watoto wengine aliodaiwa kutaka kuwapeleka msituni Chanika. 

Mrufani alishtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kufunguliwa mashtaka manne yakiwemo mawili ya kubaka na mawili ya kuingia kinyume na maumbile. 

Katika usikilizwaji alijitetea mwenyewe hakuwa na shahidi na mwisho wa shauri Mahakama ilimtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya kubaka na kifungo cha maisha kwa makosa ya kulawiti. 

Pia aliamuliwa kulipa faini ya Sh 200,000 kwa kila kosa la kubaka na fidia ya Sh 300,000 kwa kila kosa la kulawiti, pia achapwe fimbo tatu kwa kila kosa. 

Mrufani alipinga adhabu hizo akiwa na sababu mbalimbali ikiwemo Mahakama ilikosea kumtia hatiani wakati Jamhuri haikuthibitisha mashtaka dhidi yake, ushahidi wa shahidi wa kwanza na wapili ulikuwa wa uongo na si wa kuaminika. 

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Michael Lucas akisaidiana na Jenina Rugalama. 

Baada ya Mahakama kusikiliza rufani hiyo, ilibaini kulikuwa na mkanganyiko na kwamba shahidi wa kwanza na wapili walishindwa kutoa maelezo ya kina ya aliyewafanyia tukio hilo. 

"Tulishindwa kupata uhusiano wowote kati ya kukamatwa kwa mrufani Oktoba 10, 2018 na tukio lililotokea Oktoba 5,2018. Vile vile shahidi wa tano aliaminiwa na mahakama mbili za chini kwamba mrufani alikamatwa akiwa anakaribia kutenda kosa kama hilo lakini afisa wa polisi, Koplo Emmanuel ambaye alimkamata mrufani hakuitwa kama shahidi.  

"Kwa kuwa afisa aliyekamata hakuitwa kutoa ushahidi kwa sababu zisizojulikana, tunalazimika kuona kulikuwa na upungufu kwa upande wa mashtaka kwani angekuwa ameitwa ingetoa mwanga juu ya sababu halisi ya kukamatwa kwa mrufani," lilisema jopo.

Baada ya kusema hayo Mahakama ilifuta hukumu na kuondoa amri za malipo ya faini na fidia na fimbo ikiwa bado haijatekelezwa. 

Mahakama ilitoa agizo la kuachiliwa mara moja kwa Hamis, isipokuwa kama anashikiliwa kihalali kwa madhumuni mengine yoyote halali.