Yanga yakamilisha hesabu mechi CAF

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe Jumapili
Published at 08:19 AM Nov 24 2024
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.

WAKATI Mkurugenzi mpya wa Ufundi wa Yanga, Abdihamid Moallin, akikutana na wachezaji wa timu hiyo kwa mara ya kwanza, uongozi wa vigogo hao umesema wameshamaliza 'hesabu' za kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan.

Yanga itawakaribisha Al Hilal iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Florent Ibenge, katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Taarifa kutoka Yanga zinasema Moallin, ambaye hivi karubuni alitua Yanga akitokea KMC, alikutana na kusalimiana na wachezaji kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko Avic Town, Kigamboni, jijini na kufanya mazungumzo na nyota wa kikosi hicho kinachotetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mkurugenzi huyo alipata nafasi pia ya kumpa mwongozo nahodha ya kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto, ili kuhakikisha wanaenda kusaka matokeo chanya katika mechi za mashindano yote watakazocheza.

Wachezaji wa Yanga walionekana kufurahi kumwona Moallin na walimkaribisha kwa 'bashasha'.

Baadaye Moallin alisalimiana na Kocha Mkuu, Sead Ramovic pamoja na benchi lake la ufundi.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema wanafahamu mechi hiyo dhidi ya Al Hilal itakuwa ngumu na amewataka wanachama na mashabiki wao kujitokeza kuwashangilia wachezaji ili kufikia malengo.

"Ni mechi ngumu, lakini kwa ukubwa wetu na umoja wetu, wanachama na mashabiki wakiungana, wakijazana uwanjani kwa kuwashangilia wachezaji wetu, tutaifanya kuwa nyapesi, wachezaji na benchi la ufundi wapo tayari kwa vita hii," alisema Kamwe.

Aliongeza wachezaji wao watarajiwa kupambana na kuhakikisha wanampokea  kocha mpya kwa ushindi na si matokeo mengine.

"Wale waliokuwa katika vikosi vya timu ya taifa tunajua wengi walicheza kwa hiyo bado wana utimamu wa mwili, kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal, kwa maana hiyo haitampa shida sana kocha wetu, kinachotakiwa hapo ni muunganiko tu ili kupate ushindi kwenye mchezo wa kwanza ambao ni muhimu sana," alisema Kamwe.

Aliongeza hawana hofu na mchezo huo licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara na badala yake wataongeza umakini kuelekea mchezo huo.

"Hatuna hofu na mechi hii eti kwa sababu tulipoteza mechi zilizopita, badala yake imetufanya sasa tuwe makini kwenye michezo yote inayofuata, hatutadharau mechi wala hatutaingia uwanjani kwa mazoea," Kamwe alisema.

Klabu ya Yanga jana ilianza hamasa kwa ajili ya mchezo huo, huku Kamwe akiwataka mashabiki kujitokea kwa wingi Jumanne ijayo kwa ajili ya mchezo huo.

"Awali tulikuwa na hamasa ya kwenda mitandao ya kijamii, lakini leo (jana), tumeanza hasama ya mtaa kwa mtaa hadi siku ya mechi," alisema.

Tayari kikosi cha Al Hilal kimewasili nchini tayari kwa mchezo huo wa Kundi A ambalo lina timu za MC Alger ya Algeria na TP Mazembe ya DR Congo.