Yanga ndiyo basi tena

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 10:53 AM Jan 19 2025
Yanga ndiyo basi tena.
Picha: Mtandao
Yanga ndiyo basi tena.

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, jana walishindwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa suluhu na wageni MC Alger ya Algeria katika mchezo wa raundi ya sita, Kundi A, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga ilishindwa kuweka rekodi ya kuingia hatua hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo msimu uliopita na kutolewa na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilikuwa lazima ipate ushindi ili ifuzu, huku wapinzani wao wakihitaji sare tu ambayo hata hivyo waliipata.

Matokeo hayo yameifanya MC Alger kufanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifikisha pointi tisa ikimaliza mechi sita za Kundi A ikiwa nafasi ya pili na kuiacha Yanga ikimaliza nafasi ya tatu, ikiwa na pointi nane.

Vinara wa kundi hilo ambao walifuzu mapema ni Al Hilal Omduraman ya Sudan iliyomaliza ikiwa na na pointi 10 baada ya  jana kupokea kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Mazembe.

Yanga ilitawala mpira kwa asilimia kubwa jana lakini wapinzani wao walikuwa mahiri kwenye kujilinda na kuondoa hatari zote za wenyeji wao.

Dakika ya tano tu, Yanga ililisabahi lango la wageni wao, pale Stephane Aziz Ki alipompenyezea pasi safi, Clement Mzize, lakini akiwa anatazamana na kipa Abdelatif Ramdane, akapaisha mpira.

Aziz Ki, nusura aipatie Yanga bao kwa shuti kali la pembeni, baada ya kumtoka mlinzi, Mohamed Benkhemassa, lakini shuti lake kali akiwa hatua chache kutoka langoni lilipanguliwa na kipa Ramdane, kabla ya mabeki wake kumsaidia kuondosha hatari hiyo.

Boka, dakika ya 36 akiwa winga ya kushoto, aliamuacha beki wa kulia, Ayoub Abdellaoui na kupiga krosi ya ndani kidogo kwa Mudathir Yahaya ambaye licha ya kuwa kwenye nafasi nzuri, alipaisha mpira huo.

Mzize kwa mara nyingine tena akiwa umbali wa mita 30, alijaribu kupiga kombora la masafa marefu ambalo halikuwa na shabaha.

MC Alger, haikuwa na matukio mengi langoni mwa Yanga kipindi cha kwanza, zaidi ya Akram Bouras kushindwa kuunganisha krosi ya Reda Halaimia, na Larbi Tabti kujaribu kumpiga chenga kipa Djigui Diarra kwa kutumia kichwa, lakini majaribu yote hayo yalishindikana.

Kipindi cha pili, kila timu ilifanya mabadiliko, Yanga ikiwatoa Kennedy Musonda na Mudathir Yahaya na kuwaingiza Pacome Zouzoua na Clatous Chama.

Nusura Yanga ifungwe bao dakika ya 69, baada ya Tayeb Meziani kumvizia Diarra akiwa ametoka nje ya lango na kupiga mpira mrefu uliokuwa ukielekea nyavuni lakini Diara alikuwa mwepesi kurudi golini na kuzuia mpira huo usiingie.

Prince Dube nusura aukwamishe mpira wavuni dakika ya 72, alipounganisha mpira wa kona iliyopigwa na Aziz Ki, lakini kipa aliuokoa kwa mguu na kuwa kona tasa.

Dakika nne baadaye Yanga ilipoteza tena nafasi ya wazi ilipofanya shambulio kupitia kwa Aziz Ki, Pacome na Mzize ambapo shuti la Mzize liliokolewa na golikipa.