Yanga inapiga kila inayemkuta njiani

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 08:00 AM Oct 27 2024
Kiungo wa Yanga, Aziz Ki (kulia), akimtoka mchezaji wa Coastal Union, Miraji Hassan, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Kiungo wa Yanga, Aziz Ki (kulia), akimtoka mchezaji wa Coastal Union, Miraji Hassan, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana wameendeleza ushindi wao wa asilimia 100 baada ya kuifunga Coastal Union bao 1-0 katika mchezo uliochezwa, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Lilikuwa bao pekee lililofungwa na mshambuliji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jean Baleke, lililoipa Yanga ushindi na kufikisha pointi 21, ikiiengua Simba katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Yanga pia imeendeleza rekodi yake ya kutoruhusu bao lolote nyavuni kwake mpaka sasa, licha ya jana kutokuwapo kwa kipa namba moja, raia wa Mali, Djigui Diarra, badala yake alisimama, Khomeiny Aboubakar aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea, Singida Black Stars.

Kipa huyo pia ameingia kwenye rekodi ya kupata 'clean sheet' moja, huku mwenzake akiwa nazo sita.

Kona iliyopigwa na Maxi Nzengeli dakika ya 25 iliwachanganya mabeki wa Coastal Union ambao walikosea kuuokoa na kuendelea kuzagaazagaa langoni kiasi cha kutokea purukushani, kabla ya Baleke kuukwamisha mpira wavuni.

Bao hilo ni la kwanza kwa Baleke msimu huu, kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara tangu asajiliwe akitokea klabu ya Al Ittihad ya Libya.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kucheza michezo saba, ikishinda yote na kufikisha mabao 12 kibindoni, ikiwa nafasi ya pili pointi moja nyuma ya Singida Black Stars iliyo kileleni kwa pointi 22.

Hata hivyo, Singida imecheza michezo minane, hivyo iko mbele mchezo mmoja nyuma ya mabingwa hao watetezi.

Coastal ilianza kulisabahi lango la Yanga dakika ya tisa ya mchezo, kwa shambulizi la kushtukiza ambalo lingeweza kuwapatia bao kama si mpira wa kichwa cha Maabad Maulid, kugonga nguzo ya chini pembeni kulia kwa kipa, Khomeiny.

Ilikuwa ni krosi ya Ernest Malonga aliyoipiga kutoka upande wa kulia na kwenda kutua kichwani mwa mshambuliaji huyo na kuzua kizaazaa na wachezaji wa Coastal miguu yao ilionekana kuwa na kigugumizi kuukwamisha mpira wavuni.

Dakika ya 23, Coastal, ambayo karibu muda mrefu ya kipindi cha kwanza walicheza nyuma ya mpira, walirejea tena langoni mwa Yanga.

Alikuwa Maabad tena akiwa kwenye nafasi nzuri, akapiga shuti kali la chini akiwa nje ya eneo la hatari, lakini mpira uliishia mikononi mwa kipa Khomeny.

Kwa kiasi kikubwa kipindi cha kwanza hakikuwa cha kuvutia sana kutokana na Yanga kutocheza mpira wao wa kasi ambao umezoeleka, badala yake ilikuwa ikicheza taratibu, pasi fupi fupi na mara moja moja mabeki wakipiga pasi ndefu pembeni.

Angalau kipindi cha pili mpira ulichangamka hasa baada ya Yanga kuwaingiza Prince Dube, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Duke Abuya na Aziz Andambwilem kuchukua nafasi za Beleke, Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Yao Kouassi aliyeumia na Clement Mzize.

Coastal Union walikaribia kufunga, lakini Gerson Gwalala alikosa bao la wazi dakika ya 71.

Pacome naye alishindwa kupachika bao dakika nane kabla ya mpira kumalizika, baada ya kuwalamba chenga mabeki watatu wa Coastal Union, huku Dube naye akikosa dakika moja kabla ya mpira kumalizika.

Kipigo hicho kinaifanya Coastal kuteremka hadi nafasi ya 11, ikiwa na pointi nane na hii ni baada ya KMC kuichapa Prisons mabao 2-1, Uwanja wa Sokoine Mbeya hapo jana.