Vita ya kuwania nafasi ya kwanza

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 11:08 AM Jan 19 2025
Vita ya kuwania nafasi ya kwanza.
Picha: Mtandao
Vita ya kuwania nafasi ya kwanza.

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya CAF, Simba leo wanakibarua cha kusaka pointi tatu zitakazowapa uhakika wa kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Costantine.

Simba leo itavaana na vinara hao wa kundi lao kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa huku ushindi wowote utawahakikishia Simba kuibuka vinara wa kundi hilo kuelekea hatua ya robo fainali.

Ikumbukwe timu zote hizo tayari zimefuzu kwa hatua ya robo fainali na leo wapo kwenye vita ya kusaka nafasi ya kwanza.

CS Costantine wenyewe wana pointi 12 na kuongoza kundi huku Simba wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 10 wakifuatiwa na Bravo do Maquiz ya Angola na CS Sfaxien ambao wote hao hawana nafasi ya kusonga mbele.

Akizungumza kuelekea kwenye mchezo huo, Kocha Mkuu Simba, Fadlu Davids, alisema mchezo huo utakuwa mzuri na wenye upinzani mkubwa na licha ya kuwa tayari wameshafuzu amewataka wachezaji wake wapambane kusaka pointi tatu muhimu.

"Tunaenda kucheza mechi hii bila presha lakini tunahitaji kushinda,  tunafahamu tunakutana na timu ngumu katika kundi letu, mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuweza kupata ushindi," alisema Fadlu.

Aidha, alisema wanasikitika kuwakosa mashabiki wao kwenye mchezo huo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni, lakini wapo tayari kupambana kwa ajili ya ushindi. 

 "Hatutaingia uwanjani kama timu iliyofuzu, tutaingia kusaka ushindi ili kuongoza katika kundi letu, kukosa mashabiki tumehuzunika lakini dua zao ni muhimu kwetu", alisema. 

Kwa upande wake nyota wa timu hiyo, Awesu Awesu ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema wamejiandaa vizuri kwa mchezo wa leo na wapo tayari kutafuta alama tatu ili kuongoza kundi.

Kwa upande wa Kocha wa CS Constantine, Madoui Khereddine, alisema kuwa  mchezo wa leo ni fainali ya kusaka uongozi wa kundi lao.

"Sisi tumejiandaa vizuri kwa mechi ya kesho (Leo), tunatarajia kuwa na wachezaji wetu wote kwa sababu wale waliokuwa majeruhi wamepona na wapo tayari kwa mchezo huu," alisema Khereddine.

Alisema anaifahamu Simba kuwa ni timu ngumu inapocheza nyumbani, lakini kutokuwepo kwa mashabiki kumewapa unafuu wao kama wageni.

"Simba ni timu kubwa, tunaifahamu, wanakuwa wagumu sana nyumbani, tutacheza kwa tahadhari na kutokuwepo kwa mashabiki ni nafuu sana kwetu," alisema Khereddine.

Mchezo wa leo ni wa kukamilisha michezo ya hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.