TIMU ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) inatarajia kuwakaribisha Sudan katika mechi ya marudiano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Stars inahitaji ushindi wa mabao 2-0 na kuendelea, ili kuiondoa Sudan katika mashindano hayo kufuatia kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Mauritania wiki iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Stars, Bakari Shime, alisema kikosi chake kipo imara na ana matumaini ya kupata ushindi kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo wa kwanza.
"Wengi walikuwa wanacheza kwa mara ya kwanza mechi ya kimataifa, lakini walicheza vizuri mno kama ni wazoefu, tena walikuwa ugenini, hii inaonyesha wanaweza kabisa kucheza mbele ya mashabiki wao na kupata ushindi," alisema Shime.
Kocha huyo aliongeza licha ya kuwa nyumbani wanatarajia mechi hiyo pia itakuwa na ushindani kwa sababu wapinzani wao wanahitaji kusonga mbele.
Naye Nahodha wa timu hiyo, Aishi Manula, alisema wako katika mapambano licha ya Tanzania kupata tiketi ya kushiriki fainali hizo.
Manula alisema wachezaji wa timu hiyo wanataka kutumia mchezo huo kuonyesha viwango vyao.
"Tunataka kuonyesha hatima yetu nzuri ya baadaye, kuna vijana ambao wanakiu ya kufanya vizuri katika mchezo huu, tunawakaribisha Watanzania waje kufurahia ili tuwape matokeo chanya," alisema Manula.
Aliongeza watapambana kuhakikisha wanashinda kwenye uwanja wa nyumbani na sasa ni wakati wa kuondoka mawazo ya kutopata ushindi nyumbani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewataka mashabiki wengi kujitokeza kwa ajili ya kuishangilia Stars na kutangaza hakutakiwa na kiingilio chochote katika mechi hiyo.
Tanzania, Kenya na Uganda ni wenyeji wa fainali hizo mwakani, ambapo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limezipa nafasi hiyo kama majaribio ya kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2027 (AFCON 2027).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED