Mpanzu aongeza nguvu Simba CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 01:37 PM Nov 17 2024
news
Picha: Mtandao
WINGA, Ellie Mpanzu

WINGA, Ellie Mpanzu aliyesajiliwa na Simba akisubiri dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 20, mwaka huu, pamoja na kipa aliyekuwa majeruhi, Ayoub Lakred, walishuka dimbani kwa mara ya kwanza wakati timu hiyo ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC jijini, Dar es Salaam juzi.

Katika mchezo huo ambao mashabiki hawakuruhusiwa kuingia kwenye Uwanja wa KMC Complex, kwa mara ya kwanza Mpanzu alionekana kuvaa jezi nyekundu na nyeupe, mechi hiyo ikimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mashabiki wa Simba ambao walikuwa nje ya uwanja, na wengine wakichungulia kwa njia sizizo rasmi, walionekana kufurahishwa kumwona winga huyo ambaye alikuwa akiichezea klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).

Awali, Mpanzu, alikuwa asajiliwe na Simba kipindi cha dirisha kubwa, lakini dili liliharibika baada ya kwenda kufanya majaribio katika Klabu ya Genk ya Ubelgiji, majaribio ambayo hayakufanikiwa.

Baada ya kutofanikiwa na kumaliza mkataba wake wa AS Vita, Simba ilirejea katika meza ya mazungumzo na mchezaji huyo, ikampa mkataba haraka kabla ya dirisha dogo ili kuepuka kuvunjika tena kwa mchakato huo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema baada ya kuichezea kwa mara ya kwanza, Mpanzu ataanza kuitumikia timu hiyo katika mashindano rasmi kuanzia Novemba 21, mwaka huu wakati Wekundu wa Msimbazi  itakapocheza mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, utakaopigwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Lakini pia anatarajiwa kuonekana kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara itapokutana na KenGold kutoka Mbeya, mechi ikipanga kufanyika Desemba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Mbali na winga huyo Mkongomani, pia katika mechi ya juzi alionekana kwa mara ya kwanza, aliyekuwa kipa namba mmoja msimu uliopita, Lakred, raia wa Morocco.

Kipa huyo hakuonekana msimu huu kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa katika kambi ya timu hiyo nchini Misri ilipokuwa ikijiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Kutokana na kuumia kwake, mabosi wa Simba haraka walimsajili kipa raia wa Guinea, Moussa Camara ambaye kwa sasa ndiye kipa namba moja wa timu hiyo.

Lakred alionekana kuwa fiti, akifanya vitu ambavyo vimezoeleka na mashabiki wa timu hiyo akiwa langoni.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema ameomba mchezo huo wa kirafiki kwa ajili ya kuwaweka fiti wachezaji wake na kiushindani kwa sababu wanajiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis kutoka Angola utakaochezwa Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

"Tumepata mchezo huu, pia mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji pia utatupa taswira halisi ya ushindani. Tuna wachezaji ambao wapo katika vikosi vya timu za taifa, hivyo ni lazima wanaobaki nao wapate mechi za kujipima nguvu ili wote wakikutana wawe na levo moja ya fiziki," alisema Fadlu.

Taarifa zaidi zinasema Fadlu ameomba mchezo mwingine wa kirafiki kabla timu yake haijacheza mechi dhidi ya Pamba Jiji hapo Novemba 22, mwaka huu na alitamani kucheza dhidi ya Azam FC.-----------------