Kagera Sugar kutangaza 'vyuma' vyake

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 10:43 AM Aug 04 2024
Kagera Sugar
Picha: Mtandao
Kagera Sugar

KLABU ya Kagera Sugar imesema wakati wowote kuanzia kesho itaanza kutangaza wachezaji wake wapya iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kaimu Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Stephen Julius, amesema wataanza kuwaweka hadharani wachezaji wao wapya ambao anaamini wataifanyia makubwa klabu hiyo.

Alisema hayo baada ya mashabiki wa timu hiyo kulalamikia ukimya wa timu hiyo, huku baadhi ya klabu hata zile zilizopanda daraja msimu huu zikitangaza usajili wao.

Aliwaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa ukimya huo siyo kama hawajasajili, bali wameshafanya hivyo na tayari wapo kambini wakifanya mazoezi ya mwanzo wa msimu, kilichobaki ni kuwatambulisha tu.

 "Tulikuwa na mambo mengi, kwanza tulianza kikao na wazee wa mkoa, baadaye watakuja mashabiki, lakini tupo katika hatua za mwisho kabisa za kutangaza wachezaji wapya, wiki hii tunawaweka hadharani wote waliosajiliwa kuelekea msimu ujao.

Siyo kama hatujasajili, tumeshusha vyuma, wachezaji wapo kambini wanaendelea na maandalizi wadau wa soka wakae mkao wa kula," alisema Stephen.

Timu hiyo imekuwa ikifanya mazoezi ya utimamu wa mwili kwenye fukwe za Ziwa Victoria nyakati za asubuhi na jioni ikifanya maandalizi Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera.

Mashabiki wameonekana kuwa na wasiwasi na ukimya huo, baada ya timu hiyo kupoteza baadhi ya wachezaji wake muhimu baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu uliopita.

Wachezaji hao ni Ally Nassor 'Ufudu', aliyetimkia Mashujaa FC, Allain Ngeleka, kipa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliyesajiliwa na Dodoma Jiji, Mbaraka Yusuph aliyejiunga na Coastal Union, Mubarack Amza ambaye kwa sasa ni mali ya Namungo FC.