YAJAYO yanafurahisha. Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea katika reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) ambayo ujenzi wake unaendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali.
Kazi hiyo inafanyika kwa awamu kulingana na ilivyogawanywa katika vipande huku Dar es Salaam hadi Morogoro kikiwa kimekamilika na wakati wowote wananchi wataanza kutumia usafiri huo ambao unatumia muda mfupi na majaribio ya treni yameshaanza.
Kwa kawaida, usafiri wa mabasi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni takriban saa nne au zaidi lakini kwa reli ya SGR ni dakika 90 tu na itasimama vituo vyote ambavyo ni Dar es Salaam, Pugu, Soga, Kwala, Ngerengere na Morogoro. Muda huo unaonyesha kuwapo kwa faida kubwa kwa usafiri wa haraka na wa uhakika.
Muda unaotumika katika usafiri huo ni tofauti na reli ya kawaida (MGR) ambao unatumia saa tano na nusu hadi sita na nusu. Treni ya kawaida (ordinary) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, kwa mfano, unatumia saa sita na nusu wakati ile ya Deluxe inatumia saa tano na nusu.
Usafiri huo wa treni ya SGR ni wa muhimu kwa kuwa utarahisisha uafirishaji wa abiria na mizigo, hivyo kupunguza muda na hasara ambazo wananchi na wafanyabiashara wanazipata kutokana na kutumia muda mrefu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha Tabora mpaka Isaka Januari, 2023 makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema: “Lengo la serikali (kutokana na mradi wa SGR) ni kuwapunguzia wananchi muda wa safari na gharama za bidhaa kutokana na gharama za usafirishaji wa malighafi na bidhaa ili kuboresha maisha.”
Ujenzi wa kipande hicho unatarajiwa kufanyika kwa miezi 42 na kukamilika Machi, 2026 kwa gharama ya Sh. Trilioni 2.6.
Mbali na vipande hivyo, kipande cha Morogoro hadi Dodoma, ujenzi wake umefikia asilimia 97 na majaribio yameshaanza na vingine ambavyo ujenzi wake umeanza au unaendelea na kiwango cha asilimia ni Isaka –Mwanza (54.01), Tabora- Isaka (5.44), Makutupora – Tabora (14).
Ujenzi wa Tabora hadi Kigoma, unatarajiwa kuanza baada ya kumalizika kwa mvua za masika wakati cha Uvinza hadi Msongati nchini Burudi tayari mkandarasi ameshapatikana.
Mbali na vipande hivyo, kazi hiyo pia inatarajia kufanyika katika kanda ya Kaskazini, kwa maana ya kutoka Ruvu Junction hadi Tanga- Moshi na Arusha na baadaye kufika Musoma. Reli hiyo ya SGR inatarajiwa pia kujengwa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
YAJAYO YANAFURAHISHA
Kwa jicho la kawaida, watu wanafikiria katika unafuu wa usafiri na usafirishaji kutoka sehemu moja hadi nyingine katika maeneo ya mredi huo lakini kuna mambo makubwa yanayotarajiwa ikiwamo kufuka kwa uchumi na kuongeza mapato katika sekta mbalimbali.
Akizungumza hivi karibuni mafanikio ya mradi huo hasa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema kuna mafanikio makubwa kupitia mradi huo ambao hadi sasa umetumia fedha nyingi katika utekelezaji wake.
“Watu wanazungumza kwamba mradi unatumia fedha nyingi. Ni kweli lakini tusiangalie katika fedha zinazotumika bali faida zake. Kubwa Zaidi, mradi huu utafungua uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana Rais (Samia) amekuwa anatafuta fedha na kuzielekeza katika mradi. Lengo ni kuleta maendeleo ya wananchi na kuinua uchumi.
“Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi kwa nchi tunazopakana nazo ambazo hazina bandari na zinategemea bandari zetu wa ajili ya uagizaji na usafirishaji wa mizigo yao kutoka nje. Reli ya kwenda Mwanza, kwa mfano, tunalenga soko la Uganda,” alisema.
Kuwapo kwa usafiri huo utaiwezesha Uganda kupata mizigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu. Kwa mujibu wa Kadogosa, Kampala pekee hupokea tani milioni nane za mizigo kwa mwaka.
“Kwa hiyo mizigo ikifika Mwanza itakwenda na kufika haraka. Pia kutakuwa na fursa ya bandari kavu Port Bell na Jinja. Hali hiyo ipapunguza gharama kwakiasi kikubwa. Kigoma pia itaweaesha mizigo kufika Kelemie (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na kurahisisha mizigo kufika kwa haraka mashariki mwa Congo kutoka Kalemie hadi Lubumbashi,” alisema.
Kadogosa alibainisha kuwa malori ya mizigo kutoka Dar es Dar es Salaam – Bukavu hadi Goma (DRC) yanatumia siku 15. Hali hiyo, alisema inasababisha gharama kubwa kwa mzigo kufika na matokeo yake gharama za bidhaa zinakuwa juu na wanaoumia ni watumiaji kutokana na kupandishwa kwa bei za bidhaa husika.
“Baada la reli kukamilika, Dar es Salaam hadi Bukavu mzigo utafika ndani ya saa 48 (siku mbili). Hii itapunguza gharama sana. Kutoka bandari ya Durban (Afrika Kusini) hadi Katanga (DRC) gharama ya kusafirisha kontena la futi 40 ni dola za Marekani 15,000 (Sh. milioni 37.5) lakini baada ya reli, gharama yake itashuka hadi chini ya Dola 5000 (takribani Sh. milioni 12.5).
UFANISI WA BANDARI
Licha ya kunufaisha mataifa mengine, Mkurugenzi Mkuu amesema kukamilika kwa SGR kutafungua milango ya uchumi kwa bandari ya Dar es Salaam na baadaye Tanga na Mtwara kuongeza ufanisi.
“Tunatambua kwamba bandari yetu ni lango la uchumi kwa Tanzania na nchi za jirani. Kwa hiyo reli hii itawezesha bandari yetu hasa ya Dar es Salaam kuongeza ufanisi kwa kupokea na kuondoa mizigo kwa haraka.
“Kazi kubwa ya bandari ni kuuza sehemu kwa ajili ya kuweka mizigo kabla ya kuondolewa na kupelekwa inakohusika. Sasa kuwapo kwa reli ya kisasa kutafungua bandari zetu na kuwa na ufanisi na makusanyo yataongezeka mara mbili hadi tatu tofauti na sasa.
“Mizigo itakuwa inaingia na kutoka na kwa vile kutakuwa na usafiri wa urahisi na wa haraka kupitia reli, meli zitaongezeka kwa kushusha mizigo kwa muda mfupi tofauti na hali iliyopo sasa,” amebainisha.
“Lakini jambo la muhimu ni kwamba reli hii haiwezi kuwa na ufanisi kama sekta binafsi haishashirikishwa ipasavyo. Watanzania wafanye biashara na nchi zingine kupitia reli hii. Kwa kufanya hivyo, ndipo itajulikana reli hii ina maana gani kwa Watanzania. Tunaweza kuwaachia wenzetu wakaitumia ipasavyo na tukawa watazamaji,” amesisitza.
Sambamba na hilo, kiongozi huyo alisema kwa sasa mizigo mingi ya ndani na nje inasafirishwa kwa kutumia malori ambayo licha ya kuwa na gharama kubwa pia husababisha uharibifu wa miundombinu hasa barabara. Kwa mantiki hiyo, ukio wa reli ya kisasa itawezesha pia kulinda miundombinu hiyo kwa sababu mizigo mingi itasafirishwa kwa kutumia reli isipokuwa ile ambayo inakwenda sehemu ambazo hazina reli.
Pia amesema msongamano wa magari kati ya Morogoro hadi Dar es Salaam utapungua kutokana na kujengwa kwa bandari kavu eneo la Kwala mkoani Pwani. Bandari hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi hapo kicha kuchukuliwa na malori kwenda maeneo yasiyo na reli.
“Malori ya mizigo yatakuwa yanaishia Kwala badala ya kujazana katika bandari ya Dar es Salaam na hii itapunguza sana foleni katika baadhi ya maeneo Dar es Salaam. Mizigo itakuwa itakuwa inatoka bandarini hadi Kwala, pale ndipo malori yatakuwa yanachukua na kupeleka kunakohusika.
“Lakini pia tuelewe kuwa yale malori tunayoyaona yakienda Mwanza, Dodoma, Shinyanga na kwingineko yatakuwa mwisho kwa sababu mizigo itasafirishwa kwa treni kwenda huko. Kwa hiyo barabara zetu pia zitadumu na hata ajali pia zitapungua ambazo husababishwa na malori haya,” alisema Kadogosa.
WAWEKEZAJI BINAFSI
Kadogosa alihojiwa kama wawekezaji na wafanyabiashara wanaruhusiwa kuingiza mabahewa yao kama ilivyo katika reli ya sasa.
“Serikali kupitia TRC inamiliki miundombinu ya reli na mabehewa na vichwa vya treni kwa ajili ya uendeshaji. Hii haimaanishi kwamba kwa kufanya hivyo itatosheleza mahitaji ya huduma hasa usafirishaji wa mizigo.
“Kama ilivyo kwenye reli ya zamani, kuna wawekezaji binafsi kama MeTL, Bakhresa, Azania na Uganda Railway. Pia kuna vichwa vya sekta binafsi katika reli hii ya zamani.
Kwa reli mpya pia wawekezaji binafsi wataruhusiwa kuingiza mabehewa yao na vichwa. Suala si kuingiza tu bali yawe na viwango na vipimo vinavyotakiwa kulinanga na saizi ye reli na uzito wake. Watapata leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) na kanuni zinaandaliwa pamoja na operational manual (kitini cha uendeshaji) kitakamilika ifikapo Mei, mwaka huu,” amesema.
MANUFAA KWA WAZAWA
Kuna msemo kwamba ‘mgeni njoo mwenyeji apone’. Ndivyo ilivyo kwenye mradi wa ujenzi wa SGR kutokana na manufaa makubwa ambayo wameyapata.
Moja ya manufaa hayo ni ajira kwa wazawa. Kadogosa amesema tangu kuanza kwa mradi huo, ajira za moja kwa moja 31,000 zimepatikana na zingine 150,000 ambazo si za moja kwa moja.
“Ajira hizi zitachangia ukuaji wa sekta zingine kama kilimo, ufugaji na biashara,” amesema.
Manufaa mengi yametokana na wafanyakazi walioajiriwa ndani ya TRC, makandarasi na watoa huduma mbalimbali. Lakini pia tunatarajia ajira nyingi kupatikana kwa uwapo wa bandari kavu Kwala. Viwanda vitajengwa na kutakuwa na shughuli mbalimbali katika eneo lile. Mradi hii pia itachochea kwa mujibu wa Kadogosa wazalishaji wa ndani kupata fursa ya kuuza vifaa vya ujenzi kama nondo na saruji kwa ajili ya ujenzi wa reli. Alibainisha kuwa hakuna kifaa chochote cha ujenzi, hasa vile vinavyopatikana nchini, kilichoagizwa toka nje kwa ajili ya mradi.
“Kupitia mradi huu wenye viwanda vya nondo na saruji vilinufaika na vinaendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa kupitia mradi huu. Kuna kipindi itakumbukwa kulikuwa na kilio kikubwa cha uhaba wa saruji. Haikuwekwa wazi sababu ya uhaba huo lakini ukweli ni kwamba saruji nyingi ilipelekwa kwenye ujenzi wa SGR,” amesema.
Anatoa wito kwa wazalishaji wa ndani kwamba waendelee kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa kazi ya ujenzi wa reli hiyo bado ni mbichi na inahitaji vifaa vingi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED