NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema Kigoma si mkoa wa kupatia cheki namba (ajira) na kuhama kwa visingizio vya kuifuata familia au ugonjwa.
Kutokana na hali hiyo , amewataka watumishi kuachana na dhana kuwa mkoa ni wa pembezoni na hauna fursa za kiuchumi.
Sangu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwa ni kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili watumishi hao.
Alisema kwa kushirikiana na waziri wake, George Simbachawene, wameweka utaratibu wa kufanya klikini hiyo katika mikoa mbalimbali nchini baada ya kuona watumishi wengi wanalazimika kusafiri hadi Dodoma kwa ajili ya changamoto walizo nazo za kiutumishi ambazo zingeweza kutatuliwa papo kwa papo na maofisa utumishi wao.
Sangu alisema kuna dhana imejengeka kuwa mikoa ya magharibi ikiwemo Katavi, Kigoma na Rukwa kuwa ni ya adhabu kwa watumishi ambao wamepangiwa kufanya kazi katika maeneo hayo. Alisema jambo hilo si kweli ambalo hasa baada ya uboreshaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na serikali.
‘’Kumekuwa na wimbi kubwa la watumishi wa umma mara baada ya kupata ajira huja kuripoti mkoani Kigoma na kuanza taratibu za kuomba uhamisho. Jambo hili si sawa kwani wananchi wa Kigoma nao wanahitaji huduma bora kama wananchi wa Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza,’’ alisisitiza.
Alisema mtumishi wa umma atalazimika kuhama katika mkoa huo endapo atakuwa amekaa miaka mitatu na kuendelea na pia kama atakuwa amepata mtumishi mwenzake wa kubadilishana nae.
Sangu alisema Kigoma ya sasa ni bora kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu, ametoa zaidi ya Sh. trilioni 11 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwamo barabara na huduma mbalimbali kama vile afya katika mkoa huo.
Alisema kutokana na uboreshaji wa miundombinu hiyo, kwa sasa Kigoma haina tofauti na Dodoma na Arusha kwa kuwa ina kila aina ya fursa pamoja na miundombinu mizuri.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda, alisema Kigoma inahitaji watumishi wachache lakini wenye utayari wa kufanya kazi na si wale walioletwa baada ya kufanya vibaya katika mikoa mingine.
Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mbwilo Elisante, alisema mkoa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi kutokana na wengi kuhamishwa bila kuletwa mbadala.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED