Wadau wataka mabadiliko sheria ya ndoa

By Enock Charles , Nipashe Jumapili
Published at 10:56 AM Nov 17 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia (EVF), Dk  Joel Mhoja.
Picha: Enock Charles
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia (EVF), Dk Joel Mhoja.

WADAU wa kupinga ukatili wa kijinsia wameiomba Serikali kuifanyia mabadiliko Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ili kuongeza umri wa mwanamke kuolewa kuwa ni miaka 18 ili kukomesha matukio ya ukatili huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo katika zoezi la uchangiaji damu kuelekea Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani Novemba 25, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia (EVF), Dk  Joel Mhoja amesema ni muhimu kuendelea kudai mabadiliko katika sheria ya ndoa ambayo alidai inachangia katika kuongeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Kuna tafiti ambazo zimefanyika huko Zambia na Kenya zinazoonesha kwamba binti aliye na umri wa chini ya miaka 18 halafu akaolewa kwake ni rahisi kufanyiwa ukatili wa kijinsia, kwa hiyo kama wadau ni muhimu tuendelee kudai maboresho katika sheria” amesema Dk Mhoja.

Mwaka 2016 Mwanaharakati, Rebecca Gyumi alishinda kesi aliyofungua mahakamani kupinga Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na mwaka 2019 Serikali ilipewa muda wa mwaka mmoja hadi mwaka 2020 kufanyia marekebisho sheria hiyo.

Katika shauri hilo Mahakama Kuu Julai 8, 2016, ilitoa hukumu kuwa, ndoa yoyote ya mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ni kinyume cha sheria na kwamba vifungu hivyo vinaruhusu watoto kuingia kwenye ndoa wakati haifai kuwaingiza.

Dk Mhoja alisema mojawapo ya malengo ya taasisi hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia ili kukomeshwa kwa vitendo hivyo ambavyo alisema vina athari kubwa kwa waathirika na jamii.
“Lengo letu ni kuendela kutoa elimu katika jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijamii kwa sababu bado kuna watu mpaka leo wanaamini kwamba mwanamke ana haki ya kupigwa sasa ni lazima tuanze na elimu kwanza kabla ya hatua zingine” amesema Dk Mhoja

“Matukio ya ukatili ni mengi zaidi kwa watoto kuliko watu wazima kwa kiasi cha mara nane zaidi na yamekuwa yakihusisha ukatili wa kingono yakifuatiwa na kujeruhiwa katika mwili unakuta labda amepigwa na mtu ambae ni wa karibu na mengine ni ya kisaikolojia” amesema.